Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mandojo; Roho ya Mauti ni Kitendawili kigumu

Mandojo Kifoo Mandojo; Roho ya Mauti ni Kitendawili kigumu

Mon, 12 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Binadamu ni nafsi, mwili ni kasha. Una sura nzuri, mwili laini, ukiwa na nafsi katili, wewe ni mtu mbaya. Umbile lake linaweza kukutisha au uso wake ukakuogofya, ila nafsi ni njema, huyo ni mwema.

Unaweza ukaoga na kujitakasa, ukavaa nguo nadhifu na manukato ukajitwika, ukanukia uturi, ila nafsi ikiwa chafu, wewe ni mchafu. Yupo mhangaikaji wa dunia, jasho linabadili harufu ya mwili, lakini nafsi ni njema, huyo ni mtu msafi.

Moyo huakisi nafsi. Matendo mema ya mtu huwakilisha moyo wake, vivyo hivyo nafsi yake. Katili, mwovu, mfitini, msaliti na jambazi, ni zao la moyo mbaya, ndivyo ilivyo nafsi ya mhusika. Mwili ni kasha, ubinadamu ni zao la moyo, ambao ni tunda la nafsi.

Mfumo wa maisha ya mwanadamu ni kuishi na kukutana na watu. Ulimwengu ni walimwengu, jamii ni wanajamii. Hakuna jamii ya mtu mmoja. Ulimwengu utakukutanisha na walimwengu. Makutano hayo yatakuainishia watu wema, wenye ukakasi na waovu.

Mitikasi ya kiulimwengu ilinikutanisha na Joseph Francis “Mandojo”. Nikafanya naye kazi. Kitu kimoja ambacho naweza kukithibitisha ni ubinadamu wake. Alikuwa mwema, muungwana na mwanajamii mzuri.

Mandojo ni ana ya watu ambao wanaweza kukuumiza kichwa, kuwaza ni wakati gani alikuwa akikasirika. Muda mwingi ungemwona ametabasamu. Mchangamfu hasa. Ungependa kufanya naye kazi. He was an all-weather person.

Septemba 29, 2023, Alliance Francaise, Upanga, Dar, zilifanyika sherehe za Bongo Flava Honors, kutambua mchango wa Mandojo na Domokaya, kwenye ukuaji wa Bongo Flava. Ilikuwa siku bora kupitiliza. Mimi kama mwanakamati ya uandaaji na msimamizi mkuu wa maudhui na promosheni, nili-enjoy mpaka mwisho.

Mandojo na Domokaya ni professionals. Kuanzia nidhamu ya ratiba, muda hadi performance. Ni rahisi, vilevile ni burudani kufanya nao kazi.

Nipo mbali na Dar. Saa 8 mchana jana (Jumapili), napokea simu ya Mwenyekiti wa Bongo Flava Honors, Sugu The Jongwe. Akanijulisha: “Kuna habari mbaya. Mandojo ameuawa.” Mazingira ya kifo yanaumiza zaidi.

Dojo hanywi pombe kabisa, eti siku ya tukio alikunywa. Akahisiwa ni mwizi, akauawa. Roho ya mauti ni kitendawili kigumu ajabu.

Usiku mwema, Brother.

Ndimi Luqman MALOTO

Chanzo: www.tanzaniaweb.live