Shinyanga. Majonzi na simanzi vilitawala katika ibada ya mazishi ya Charles Kanumba ambaye ni baba mzazi wa aliyekuwa mwigizaji maarufu wa filamu nchini Tanzania, Steven Kanumba.
Ibada hiyo imefanyika leo jioni Jumanne Februari 10, 2020 nyumbani kwake mtaa wa Magadula kata ya Ngokolo na kuongozwa na mchungaji wa Kanisa la AIC, Zabron Mangwengula aliyewataka waombolezaji kutenda mema.
TANZIA: Baba wa Kanumba afariki
Zabron amesema maisha ya Charles yalikuwa mikononi mwa Mungu kwa kuwa binadamu wanaishi kwa uwezo wake, “hakuna anayejua siku wala saa. Binadamu anapaswa kujiandaa muda wote kwa kusali na kufuata mafundisho ya Mungu.”
“Tunapokuwa hai tuna faida mbele ya jamii inayotuzunguka na ndio maana leo hii watu wanalia kwa uchungu kutokana na upendo mkubwa alikuwa akiuonyesha mzee wetu ambaye leo tunamuaga na kwenda kumpumzisha kwenye nyumba yake ya milele,” amesema.
Akisoma wasifu wa Charles, Reuben Zakayo amesema alizaliwa mwaka 1949 Kwimba mkoani Mwanza na ana watoto tisa lakini wawili wa kiume wameshafariki dunia.
Pia Soma
- Uhakiki vyama vya siasa wawaibua wanasiasa, Mutungi awajibu
- Chadema wachangishana fedha usiku kuwatoa kina Mbowe rumande-VIDEO
- MPYA: Mbowe, wenzake washindwa kulipa faini Sh350 milioni, kulala rumande-VIDEO
Amewahi kufanya kazi ofisi ya mkuu wa Mkoa Shinyanga idara ya utamaduni, amewahi kuwa ofisa mtendaji wa kata ya Mwawaza, Kambarage, Ndala na hadi anastaafu mwaka 2015 alikuwa kata ya Chamaguha.
Mwenyekiti wa mtaa wa Magadula, Hamphrey Mtafungwa amesema wamepoteza kiongozi aliyekuwa mshauri katika jamii iliyomzunguka.
Maziko yatafanyika kesho Jumatano Machi 11, 2020 katika kijiji cha Nyakaboja Nasa wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Steven Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012.