Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ingekuwa vipi Mwana FA angekuwa Waziri wa Fedha?

Waziri Chana Asisitisha Ushirikiano Akimpokea MwanaFA Wizarani.jpeg Ingekuwa vipi Mwana FA angekuwa Waziri wa Fedha?

Mon, 6 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ingekuwa vipi Dully Sykes angeimba hardcore, mashairi kama Jay Moe, neno Mwanasesere naimani lisingekuwepo, mauzo ya Rap Bongo yangefika platinum tano.

Ndivyo alivyokuwa akiwaza kwa kina Hamisi Mwinjuma 'Mwana FA' katika wimbo wake 'Ingekuwa Vipi' ambao ndio uliomtoa kimuziki miaka zaidi ya 20 iliyopita.

Wimbo huo aliomshirikisha Jay Moe ulitoka Februari 2, 2002 na ulioredidiwa Mawingu Studio na DJ Bonny Love, FA na Moe kwa pamoja alikuwa wanajenga hoja kwenye mambo ambayo kama yangetokea, ingekuwa vipi.

Mwana FA ambaye ni Mbunge wa Muheza, Tanga, sasa ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, aliteuliwa na Rais Samia Suluhu kutumikia nafasi hiyo Februari 26, 2023 na siku iliyofuata akaapishwa.

Hata hivyo, ingekuwa vipi kama Mwana FA angeteuliwa Wizara ya Fedha na Mipango?, hiyo ni kutokana katika nyimbo zake nyingi amekuwa akiitaja fedha, pengine ndiye msanii aliyefanya hivyo mara nyingi zaidi.

Kwa miaka 21, tangu mwaka 2003 hadi 2022, Mwana FA ametoa nyimbo zaidi ya 10, wastani wa wimbo mmoja kwa kila baada ya miaka miwili ambazo zote amekuwa akiitaja fedha kwa namna ya kuitafuta, kuitunza na kutoiabudu. Hizi ni baadhi ya nyimbo hizo;

1. Binamu (2003) Ni wimbo unaopatikana kwenye albamu yake ya pili, Toleo Lijalo (2003) baada ya Mwanafalsafani (2002), alikuja kuurudia kurekodi na Marco Chali ndani ya Kama Kawa Records na ndio wimbo uliomtambulisha Chali Bongo kama Prodyuza.

"Mimi ni msafi kama pesa mpya, zidisha wazo upya" anachana Mwana FA katika verse ya pili, katika verse ya tatu anaongeza kitu kinachoshabiana na fedha, "Walishatabiri kwamba nitakufa tajiri, so punguzeni maswali ninapokamata vivuli,".

2. Nazeeka (2009) Kwa sasa tunaweza kusema ni wimbo uliokutanisha wabunge watatu tena wanaofanya Hip Hip, kuna Mwana FA, Profesa Jay na Sugu ambaye naye anaigusia fedha kwa kusema; bado nakula kuku, milioni kwangu ni buku!.

"Napenda mkwanja zaidi navyopenda bifu, naangalia biashara naona nazeeka sasa... Siku hizi milioni milioni ndio zinaniumiza ubongo," anachana FA katika ngoma hiyo iliyotengenezwa na Hermy B.

3. Msiache Kuongea (2009) Ni wimbo wa mwisho kutoka rasmi ambao Mwana FA kashirikiana na Lady Jaydee baada ya Alikufa kwa Ngoma, Sitoamka, Hawajui, Wanaume Kama Mabinti na Sikiliza wake Ngwea.

"Nimewekeza miaka kibao kuwa hapa nilipo mwana, sikuzaliwa kwenye mali ilibidi kuhangaika sana, sio mambo safi pua zangu zinanusa mkwanja," anachana FA katika ngoma hiyo iliyotengenezwa B'Hits na Hermy B.

4. Unanijua Unanisikia (2011) Ukiwa fukara kamwe huwezi kuwa kiburi, masikini jeuri ni msemo tu usiuweke kwenye akili. Ni mstari wa kwanza wa Mwana FA katika wimbo wake 'Unanijua Unanisikia' ambao unauita "Money Script" kutokana ameizungumzia sana fedha.

"Hela hazilali so ukilala wewe tu, na zina kasi ya kutengenezwa hazikungoji uamke mkuu. Me na make money mchana na make money usiku, iwe kwa tai au kwa jeans me naingiza mkwanja babu. Naingiza mkwanja najua na naingiza totoro, mwenzangu sio unazibagua me sina nazo mgogoro," anachana FA katika ngoma hiyo iliyosimamiwa na Hermy B toka B'Hits.

5. Mfalme (2014) Kuna vingi vya kumuomba Mungu kabla hujamuomba utajiri. Anasema Mwana FA katika wimbo wake, Mfalme akimshirikisha G Nako, huu nao kagusia na namna alivyopamba kuipata fedha.

"Sina hata mia ya urithi vyote hivi ni vya kwangu, nishaenda shule bila viatu, nishatoa funza kama buku, na ipo siku utaniheshimu ama utaheshimu hela zangu!," anachana Mwana FA katika ngoma hiyo iliyotengenezwa na Nahreel na Marco Chali.

6. Kiboko Yangu (2014) Hata kwenye nyimbo za mapenzi, bado Mwana FA inaitaja fedha tu, katika wimbo wake 'Kiboko Yangu' uliopikwa MJ Records na Marco Chali akimshirikisha Alikiba, anamtaja mkewe kama ndiye mtunza fedha zake.

"Huwezi omba ndege una akili, huwezi omba meli. We ndio mtunza hela zangu, utaomba unachoweza himili," anachana Mwana FA katika wimbo huo ulioshinda tuzo Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) 2015 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana.

7. Asanteni kwa Kuja (2016) Katika verse ya tatu ya wimbo wake, Asanteni kwa Kuja, Mwana FA anaitaja fedha kama chanzo cha uvunjifu wa amani na mvurugano hata kwa watu ambao mwanzo waliishi kwa maeleweno ila ni muhimu kuisaka na kuwa mtulivu.

"Siku nyingine, hela nyingine... We get money on the right things, and keep calm, wenye kelele wote sio Kings, kuwa na nidhamu,"  anasema Mwana FA katika wimbo huo uliotengenezwa B'Hits na Hermy B.

8. Upo Hapo? (2017) Ni ngoma nyingine kutoka B'Hits katika mikono ya Hermy B, imewakutanisha Mwana FA, AY na Fid Q, kama kawaida FA kaigusia fedha, licha ya kuwa na dili za mabilioni kwake kuvaa tai sio jambo lenye ulazima.

"Dili za mabilioni na bado tai huzioni, winning together wanangu begani," anachana Mwana FA ambaye katika video ya wimbo huo anajitambulisha kama 'The Godfather', huku AY akitumia 'The Butcher' na Fid Q 'Lord of War'.

9. We Endelea Tu (2018) Wimbo huu uliotengenezwa na Abby Dady, Mwana FA kazungumzia fedha kwa hasira sana, anataka fedha iheshimiwe baada ya dini, sio kucheza nayo kwa kujionyesha kwa watu.

"Hela zinafanya dunia inazunguka let me handle this.... Tafuta hela za kutosha ila isipinge nazo picha, maisha yanabadilika, kausha nitakufundisha.... Heshimu pesa baada ya dini, kwenu hakuna wakubwa wangekuwepo ungeniamini," anachana Mwana FA.

10. Sio Kwa Ubaya (2022) Mwana FA anaanza katika wimbo huu aliomshirikisha Harmonize kwa kueleza kuwa fedha sio makalio kamba kila mtu awe nazo, hivyo kuwaza fedha hakuna kwenda likizo hasa kwa wenzake ambayo hawakuzaliwa nazo.

"Penda hela husiziabudu, husivukwe na utu.... Pesa hainunui furaha ufukara unanunua nini, mi nakimbiza hela mademu nawaachi ninyi... Pata hela maadui zako wanune... Mpunga ndio nguvu za kiume" anasema FA ngoma hiyo iliypikwa na Gachi B.

Ukiachana na hizo, nyimbo nyingine ambazo Mwana FA kazungumzia fedha ni; Habari Ndio Hiyo na Bila Kukunja zote akiwa na AY, Dume Suruali akimshirikisha Vanessa Mdee n.k.

Ikumbukwe Mwana FA alianza kujifunza muziki kupitia kundi la Quite Gangsters Chronic (QGC) Dar es Salaam, alipoenda Tanga kusoma akajiunga na kundi la Black Skin ambao washindani wao walikuwa ni Raff Niggaz. Jina la Mwanafalsafa (Mwana FA) alipewa na DJ Bonny Love  baada ya kurekodi wimbo wake, Mwanafalsafa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: