Dodoma. Wasimamizi wa mirathi ya wasanii marehemu Steven Kanumba na King Majuto wamelipwa Sh45 milioni baada ya kamati ya kupitia mikataba ya wadau wa filamu iliyoundwa na Serikali kufanya kazi ya kupitia upya mikataba ya wasanii.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Aprili 18, 2019 na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Amesema kufuatia tangazo la wizara kupitia upya mikataba mibovu waliyoingia baadhi ya wasanii na hivyo kuathiri kipato chao, kamati ya kupitia mikataba ya wadau wa filamu iliundwa na kuchambua mikataba 11 iliyowasilishwa.
“Baadhi ya kampuni zimethibitisha kuwalipa wahusika viwango vya kuridhisha na nyingine zimeingia kwenye makubaliano maalum na kamati ya kuongeza viwango mbalimbali,” amesema.
Ametoa mfano kampuni za Pan Afrika Enterprises Ltd na Ivori Iringa zimeingiza kwenye akaunti maalum Sh 30 milioni kwa kazi alizotekeleza marehemu King Majuto kimkataba.
“Kampuni ya Azam-SSB imeandaa malipo ya ziada ya Sh 20 milioni na kampuni ya Tanform ya Arusha Sh 15milioni ambayo yatawasilishwa kwa msimamizi wa miradhi ya marehemu King Majuto,” amesema.
Amesema pia baadhi ya kampuni ikiwamo Neelkanth Salt Ltd zimejiwekea utaratibu wa kuridhisha wa mawasiliano ya moja kwa moja na familia ya King Majuto.
Dk Mwakyembe amesema pia kampuni ya Steps Entertainment imemkabidhi mama wa marehemu Steven Kanumba ziada ya Sh 15 milioni na kwamba kampuni hiyo imeahidi kushirikiana naye kuandaa filamu ya maisha ya mwanawe.
Kampuni hito pia tayari imemlipa msanii Sikujuwa Mbwewe Sh 6.7 milioni kutokana na kusambaza filamu yake inayojulikana kwa jina la Utu Wangu bila ridhaa yake na filamu hiyo imerejeshwa.