Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ditto kukata rufaa kesi yake na DStv

Lameck Ditto Eds Ditto kukata rufaa kesi yake na DStv

Thu, 25 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwimbaji wa muziki Lameck Ditto ameamua kukata rufaa kupinga hukumu ya kesi ya madai dhidi ya Kampuni ya Multchoice Tanzania Limited maarufu DSTV.

Ditto ambaye jina lake halisi ni Dotto Bwakeya, alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam mwaka 2020 akiiomba iamuru DSTV imlipe fidia ya Sh6 bilioni kwa kutumia wimbo wa Nchi Yangu aliodai ni wake kwenye matangazo yao ya biashara bila ridhaa yake wakati wa kampeni za  fainali ya Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2019.

Pia aliiomba Mahakama iamuru alipwe Milioni 200 kutokana na madhara ya jumla, pia alipwe riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo akidai kampuni hiyo imemnyima fursa ya kunufaika na kazi yake.

Naibu msajili wa Mahakama hiyo, Mery Moyo alisoma hukumu hiyo jana Julai 23, 2024, hukumu iliyotolewa na jaji mfawidhi wa mahakama hiyo, Salma Maghimbi ambaye hakuwepo Mahakamani juzi.

Moyo aliyepewa jukumu la kuisoma tu hukumu, alisema mahakama imeshindwa kumtia hatia mdaiwa (DSTV) kwa kuwa wimbo uliotumiwa na DSTV sio orijino ambao  Ditto ndiye mmiliki.

Moyo alianza kusoma hukumu hiyo iliyokuwa na kurasa 10 kwa kueleza imetolewa na jaji Maghimbi na yeye amepewa kuisoma tu na kuanza kwa kueleza katika uumbaji Mungu ametoa karama mbalimbali ambazo ndiyo chanzo cha kipato na mali.

Alifafanua maana ya haki miliki akisema ni neno la kisheria linalotumika kutafsiri haki ya anayetengeneza kazi fulani akizichanganua kazi hizo ikiwamo ya muziki na kuendelea kwa kusema.

“Hakimiliki inatunza kazi ya asili ambayo imetengenezwa, ingawa inaweza kutunzwa pale tu inapotengenezwa na kusajiliwa, kabla ya kueleza mwenendo wa kesi ulivyokuwa kisha kueleza Mahakama imeshindwa kumtia hatiani mdaiwa kwa kuwa alitumia wimbo wa Nchi yangu toleo la pili ambao Ditto si mmiliki wake ikimtaja Ditto kama mmiliki wa tolea la kwanza tangu mwaka 2019.

Nje ya Mahakama hiyo, Ditto alisema hakubaliani na hukumu iliyotolewa na anachokisubiri ni nakala ya hukumu ili akae na wanasheria wake na kufanya uamuzi mwingine wa rufaa.

“Uamuzi uliotolewa umenishangaza, kama Mahakama inasema wimbo orijino ni wangu, na DSTV  imetumia second version (toleo la pili) ambao  tulifanya kwenye urithi festival  (tamasha la urithi) hivyo imeshindwa kumtia hatiani mshitakiwa kwa kuwa alitumia version ya pili, hiyo version ya pili ni ya nani?,” alisema Ditto kwa uchungu.

Alisema katika suala la hakimiliki ya wimbo mwenye haki ni mbunifu na umiliki wake unaondoka kama amemmilikisha mtu mwingine kwa maandishi na mikataba, yeye (Ditto) hakufanya hivyo.

“Naelewa gharama ya kupambania haki ni kubwa na mimi sitoacha kupambania haki yangu kwa namna yoyote ile,” alisisitiza Ditto.

Mwanasheria wa DSTV, Simon Lyimo aligoma kuzungumza chochote baada ya hukumu hiyo huku yule wa Ditto, Samson Lukumay akieleza wamepokea uamuzi wa Mahakama na wataipitia nakala ya hukumu na  kukaa na mteja wao kuona utaratibu wa kukata rufaa.

Katika kesi hiyo, wakati wa ushahidi Ditto alipeleka mashahidi watano,  na DSTV ilikuwa na mashahidi wawili, Astrid Mapunda na Johnson Mshana wakiongozwa na mawakili, Simon Lyimo na Thomas Mathias.

Upande wa Ditto, baadhi ya mashahidi walikuwa ni produzya wa wimbo huo, Emmanuel Maungu (Emma the boy), meneja  Rodney Rugambo na Angela Karashani wakiongozwa na mawikili, Ally Hamza, Elizabeth Mlemeta na Lukumay.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live