SUPASTAA Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ametoa kauli ya kumlinda msanii mwenzake Ali Saleh Kiba ‘AliKiba’ ambaye Watanzania wanaamini ni hasimu wake mkubwa, RISASI linakupa ubuyu kamili.
Diamond au Mondi ametoa kauli hiyo juzikati kwenye hafla ya Komunio ya Kwanza ya mtoto wa muigizaji Irene Uwoya, Krish Ndikumana iliyofanyika katika Ukumbi wa Hekima Garden, Mikocheni jijini Dar.
NI MAHOJIANO
Akifanya mahojiano na vyombo vya habari ukumbini humo, Diamond alianza kwa kueleza muziki wake na kusema kwamba amekuwa kimya kwa muda mrefu lakini sasa hivi anajiandaa kuachia albamu yake ambayo kwa kiasi kikubwa imekamilika.“Mimi sijatoa ngoma toka mwaka jana, nadhani nina zaidi ya miezi sita sasa sijatoa ngoma.
Mwaka jana yenyewe nimetoa nyimbo mbili tu lakini nashukuru Mungu zinafanya vizuri mpaka sasa kwenye mauzo,” alisema Mondi.
UTARATIBU WA MONDI
Diamond aliongeza kuwa, hatoi tu nyimbo ili mradi bali huwa anaandaa mikakati mizuri kabla kuachia na ndio maana nyimbo zake zimekuwa zikifanya vizuri ambapo nyimbo hizo mbili alizoziachia mwaka jana, ndio zinaongoza mpaka sasa kwa kutazamwa YouTube.
KUMLINDA KIBA
Kwenye mahojiano hayo, mkali huyo anayetamba na wimbo wa Waah aliomshirikisha Koffie Olomide, alipata wasaa wa kuzungumzia kauli mbiu yake kwa sasa ya Swahili Nation na hapo ndipo aliposema, yuko tayari kumlinda AliKiba pamoja na wasanii wengine.
Alisema Swahili Nation ni wazo ambalo lilimjia baada ya kuona mataifa mengine, wanakuwa na umoja wa kujitambulisha kama watu wa jamii fulani hivyo na yeye ameona kama Watanzania pamoja na nchi za jirani ambazo zinazungumza Kiswahili, zisimame pamoja.“Mimi naamini katika positivity, napenda tuwe na kitu chetu kama ambavyo wenzetu wanasimama mfano Sauz Afrika na kwingineko. Ukifika ukamzingua mtu wa jamii fulani basi ujue watakuzingua,” alisema Mondi.
ANACHOTAMANI KUKIONA…
Alisema, anachotamani kuona ni kwamba kila mtu ambaye anazungumza Kiswahili basi awe balozi mzuri wa kutetea Uswahili kwa kusimama imara kulindana kama wasanii au jamii nzima inayozungumza lugha hiyo ya Kiswahili.“
Yani mimi hapa siko tayari kuona Alikiba anazinguliwa halafu mimi nikakaa kimya, ukimzingua Alikiba nakumainindi kwamba kwa nini umzingue?
Ukimzingua mtu kama Ben Pol au msanii yeyote yule mimi lazima nimtete kwa hiyo hiyo ndiyo Swahili Nation ninayotamani kuiishi,” alisema Mondi.
AKITAJA KIFO
Staa huyo ambaye ndiye bosi wa Wasafi FM na Wasafi TV, alisema kwenye maisha yeye anaamini katika misingi ya kuishi kwa kutokuwa na kinyongo na mtu kwani duniani kila mwanadamu anapita, kila mtu atakufa.
Alisema, kwenye kuamini misingi hiyo ndio maana pia alisamehe yote yaliyopita kwenye ugomvi wake na mtangazaji Loveness Malinzi ‘Diva’ ambaye hivi karibuni amejiunga na timu ya Wasafi FM licha ya kuwa kwenye bifu kali miaka kadhaa iliyopita.
Alisema haoni sababu ya kugombana na mtu au kuishi na kinyongo na kwamba atazungumza hilo kwa kirefu zaidi hivi karibuni atakapoalikwa na Diva katika kipindi chake cha masuala ya mahusiano.
“Nitazungumza zaidi kwenye kipindi, sijazungumza kuhusu mahusiano muda mrefu hivyo kupitia kipindi hicho nitazungumza pia,” alisema Diamond.
TUJIKUMBUSHE
Mondi na Kiba kwa muda mrefu wamekuwa mahasimu ambapo mara kadhaa wamekuwa kwenye vita ya maneno ambapo mara nyingi Kiba ndio amekuwa akimrushia mwenzake vijembe lakini Diamond yeye huwa anazungumzia zaidi umoja na maelewano kati yao.
MWANDISHI WETU, RISASI