Msanii wa filamu Bongo, Gabo Zigamba amesema kuonekana kuna pengo la Marehemu, Steven Kanumba katika tasnia hiyo ni kutokana na kutoanda vijana wengi wenye uwezo kama aliokuwa nao.
Muigizaji huyo ameshauri kwa sasa ni muda kwa Bongo Movie kuandaa vijana wengi wenye uwezo mkubwa ili kusije kukajitokeza kitu kama hicho siku za mbeleni.
“Ukiachilia mbali Kanumba alikuwa kipenzi cha watu alikuwa ni mmoja ya watu ambao wanaleta ushindani, watu walikuwa wanajifunza kupitia yeye,” amesema.
“Sasa baada ya yeye kuwa amefumba macho amekwenda kwenye ahadi ya Mwenyenzi Mungu, ni sawa na timu ambayo inakosa namba sita, ni rahisi kufungwa. Kwa hiyo watu wajipange kuwaanda namba sita wale wengi kwa roho nzuri, kuna uwezekano mapengo kama yale yasitokee tena,” Gabo ameiambia Bongo5.
Gabo ni miongoni mwa wasanii wa Bongo Movie ambao wanafanya vizuri zaidi kwa sasa. Usiku wa April 01, 2018 alishinda tuzo tano za Sinema Zetu International Film Festival Awards (SZIFF).