Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayoyapitia mjane wa Mzee King Majuto

Majuto Mkee (1) Anayoyapitia mjane wa Mzee King Majuto

Sat, 13 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

"Tangu afariki marehemu mume wangu mpaka leo, si muangaliaji wa tamthilia wala filamu ya mtu yeyote, kwa sababu unakuta filamu nyingi anakuwa ameshiriki, kwa hiyo ukija ukimuangalia unamuona, majonzi  yanarudi tena, labda naweza kuangalia hizi za Kituruki huwa napenda sana.”

Huyo ni Aisha Mbwana, mjane wa aliyekuwa msanii maarufu nchini Tanzania, King Majuto akielezea maisha yake baada ya kifo cha mume wake, kati ya mambo ambayo yamemuathiri ni kuangalia filamu zake kwa sasa hawezi tena.

Agosti 8, 2018 majira ya saa 1:30 usiku, Watanzania walipokea taarifa ya kushtua kuhusu kifo cha msanii Amri Athuman au King Majuto kama alivyozoeleka na wengi, aliyefariki dunia wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Inaelezwa kuwa chanzo cha kifo cha mzee Majuto ni ugonjwa wa tezi dume ambapo alisafirishwa kwenda nchini India kupatiwa matibabu na baadaye kurudi, akawa anaendelea na kliniki yake Muhimbili hadi kifo kinamkuta.

Maisha ya King Majuto katika familia yake

Mjane huyu wa King Majuto anasema mume wake alikuwa na wake wawili na mmoja alishatangulia mbele ya haki, ila kwa ujumla King Majuto alijaaliwa kupata watoto 15, watano kati ya hao wamefariki dunia.

Anasema watoto wake wengi ni wasanii kama baba yao na wanapambana kwenye shughuli za uigizaji, licha ya kwamba pia wanafanya na shughuli zao nyingine na sababu kubwa alikuwa akiwashirikisha kwenye baadhi ya kazi zake.

“Wakati wa maisha yake King Majuto alikuwa ni mtu wa masihara na mcheshi sana hata anapokuwa nyumbani na alipenda sana watu, ila akiwa nyumbani anabaki kama baba na kusimamia majukumu yake vizuri na sio mkasirikaji,” anasema.

  Mtoto wa pili wa King Majuto akiomba dua kwenye kaburi la baba yake

Lakini kingine anasema King Majuto alikuwa mtu ambaye anapenda kufanya ibada na mchapakazi hali ambayo hawezi kukaa nyumbani bila kufanya kazi yoyote.

Moja ya shughuli kubwa ambayo alikuwa anapenda kuifanya akiwa nyumbani ni ufugaji hasa wa kuku, hivyo kusafisha mabanda ya kuku na kuwalisha ilikuwa ndiyo kazi yake kubwa na baadhi ya wajukuu zake.

“King Majuto alikuwa ni mtu wa watu, kwanza alikuwa anapenda watu sana, ni mtu wa masihara yaani kwa wastani alikuwa siyo mkasirikaji mara nyingi ni mcheshi mbele za watu, kiufupi yeye alikuwa mpenda ibada na mchapakazi, alikuwa hapendi kukaa alikuwa akijishughulisha na shughuli mbalimbali,” anasema Aisha Mbwana.

Mke azuiwa kuigiza

Katika maisha ya kawaida ya kuigiza, mzee Majuto baada ya kuigiza filamu kadhaa na mkewe baadaye aliamua kumkataza asiendelee na uigizaji na kumtaka kubaki nyumbani kulea familia.

Mjane huyo anasema aliwahi kuigiza na mume wake miaka ya nyuma kabisa kwenye filamu ambayo ilipewa jina la “Fukara Hatabiriki” ila baadaye katika kuonekana mabadiliko ya kuingia maisha ya kisasa akamwambia apumzike.

Mke wa King Majuto

“Maadili yalipoanza kubadilika tu akaona hapana na wewe mke wangu unaweza kufuata zile nyendo ambazo mimi sikupenda, kwa wastani sasa hivi wasanii wamebadilika, maadili yao yamekuwa siyo mazuri katika mavazi wakati mwingine katika matamshi, hawaangalii zile kazi zinakwenda kuangaliwa na watu tofauti, ina maana leo hukai sebuleni na mkwe wako mkaangalia tamthilia, lazima utaondoka, ningewaomba wabadilike,” anabainisha.

Anasema changamoto hiyo ya kubadilika kwa maadili katika kazi za sanaa marehemu King Majuto alianza kuiona mapema, ila kusimama peke yake kuanza kukemea haikuwa rahisi, hivyo alikuwa akiongea na msanii mmoja mmoja kuhusu kulinda maadili na hata ukitazama wale ambao walikuwa karibu yake walikuwa vizuri.

Anasema wasanii wameacha maadili na kanuni za mila na desturi za kitanzania katika kufanyakazi zao na badala yake wanaiga zaidi mambo ya nchi za ulaya katika mavazi, lugha na matukio mengine ambayo yanaharibu utamaduni wa Tanzania.

“Wasanii wavae mavazi ya kujistiri wanapokuwa kwenye kazi zao za uigizaji, lakini pia katika kutamka baadhi ya maneno yawe kwenye tafsida ambazo zinaficha uhalisia, ila kwa wakubwa wanaelewa hilo neno, ila siyo kuiga uzungu na kila kitu kwenda kama kilivyo, hapana, hili linabomoa utamaduni wetu kama Watanzania,” anasema.

Mtoto aeleza maisha ya baba yake na chimbuko lao Mtoto wa pili wa King Majuto anayefahamika kwa jina la Mohamed Amri ambaye pia anajishughulisha na uigizaji anasema wao wamezaliwa na kukua katika Mkoa wa Tanga na kihistoria baba yao pia ni mzaliwa wa Tanga, lakini kiasili babu zake ni  Wamanyema wa Kigoma, waliahamia Tanga na hawakurudi tena Kigoma.

Mohamed amesema katika historia aliyopewa baba yake alianza kuigiza akiwa na umri wa miaka 13, akiwa shule ya msingi mpaka anamaliza masomo yake ya sekondari ya darasa la nane akiwa na kipaji hicho cha kuigiza, aliendelea hivyo katika maisha yake yote mpaka anafariki dunia.

Historia ya King Majuto inaeleza kuwa alipomaliza masomo ya sekondari darasa la nane alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa enzi hiyo likiwa chini ya Serikali ya Kijerumani lakini mwaka 1979 aliacha kazi jeshini.

Mohamed anasema baada ya kuacha kazi jeshini, King Majuto alijiunga na kufanyakazi bandarini katika kitengo cha zimamoto, ambapo alifanya huko kama askari wa zimamoto mpaka pale alipoamua kuacha tena na kutafuta shughuli nyingine.

“Lakini kote huko wakati anapita alikuwa ni msanii, hivyo anaingia kama msanii isipokuwa jeshi hakuingia kwa nafasi hiyo ya usanii, baada ya hapo ndiyo akaingia rasmi kwenye makundi ya uigizaji jijini Dar es Salaam ikiwemo Tanzania One Theater  (TOT), Muungano Cultural Group na vikundi vingine,” anasema Mohamed. Kadhalika katika shughuli zake za uigizaji mzee Majuto aliwawahi kufanyakazi na vituo vya televisheni, kampuni mbalimbali kama za kutengeneza magodoro, kuzalisha chumvi na nyinginezo.

Kauli ya jirani anayeishi kwenye shamba la King Majuto alipozikwa

Mkazi wa Kijiji cha Kiruku, Rehema Amiri alikuwa jirani wa King Majuto ambaye amepewa nyumba na marehemu, ameeleza maisha waliyoishi na msanii huyo na kusema yapo mambo mawili alimuagiza kufanya muda mchache kabla ya kifo chake.

Amesema siku moja aliitwa na Majuto nyumbani kwake Donge na alipofika alimueleza kwamba amefikiria akijifungua mtoto wake ampe jina la King Majuto na aliporudi kijijini alimfikishia ujumbe huo mume wake, wote walikubali ombi hilo na kumpa mtoto wao jina la Majuto.

“Nilipofika akaniambia mimi nataka niondoke nikafanyiwe upasuaji lakini nilichokuitia ni  mwanao  ndiyo King Majuto, na huyu ndiye atarithi mambo yangu, kwa hiyo hilo jina ambalo mmetoka nalo huko kwenu mtabaki nalo ila nataka aitwe King Majuto, ndio hicho nilichokuitia, nikamwambia sawa,” anasema Rehema.

Anasimulia kuwa tukio lingine kabla ya kifo chake King Majuto alifika shambani hapo na kumuonyesha eneo ambalo akifa alitaka azikwe. Jambo ambalo alidai lilimshtua lakini alikubaliana nalo, kwa kuwa ni kama agizo hivyo alilifikisha kwa wengine baada ya kifo kutokea.

“Neno la mwisho anaondoka aliahidi kwamba mimi nikifa kaburi langu kiwanja changu ni hiki hapa kwa hiyo yeyote atakayekuja, mtamwambia hivyo kwamba mimi nazikwa hapa na wala msitetereke, baada ya kuniambia maneno hayo wakapanda kwenye gari wakaondoka kwenda Dar, baadaye naambiwa kazidiwa hata sijakwenda kumuangalia, akafariki dunia,” anasimulia Rehema. 

Kauli ya Chama cha Waigizaji Tanga kutokana na kifo cha King Majuto

Katibu wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Tanga, Raphael Kiango amesema kifo cha King Majuto ni pengo kubwa kwao, kwani aliweza kuibua vipaji lakini pia kuviendeleza yeye mwenyewe, kwa kuwashirikisha wasanii kwenye filamu mbalimbali.

Amesema kuna wakati King Majuto akihitajika kufanyakazi na wasanii wengine, alikuwa akiwashawishi kwenda mkoani Tanga na kuwahakikishia kuwa wasanii wapo na mazingira ya kufanyiakazi yanapatikana, hivyo ilikuwa ni fursa kwao na wadau wengine wa filamu.

Alidai tangu afariki dunia 2018 hata idadi ya wasanii wageni waliokuwa wanafika mkoani Tanga wamepungua na changamoto kubwa hakuna msukumo kama ule ambao alikuwa anaufanya marehemu kwa kuwavuta wasanii wenzake kuja Tanga.

“Mzee alikuwa ni mtu wa kutufundisha jinsi ya kuishi maisha ya nje ya sanaa, kuishi na watu vizuri pamoja na kujenga mtandao mpya wa kuweza kufanyakazi na wengine, lakini alikuwa akitutafutia fursa kwa waigizaji wenzake wanapokuja Tanga, hili ndiyo kubwa zaidi kwetu ambalo kwa sasa tunalikosa kutokana na kifo chake,” anasema Kiango.

Mipango ya kumuenzi King Majuto kwa wasanii na familia ikoje? Mjane wa King Majuto anasema kila ifikapo Agosti 8, wamekuwa wakifanya dua maalum nyumbani kwa marehemu katika Kijiji cha Kiruku, ambapo wanakutana wadau mbalimbali na kufanya dua na utoaji wa sadaka.

Hivyo amewakaribisha wasanii wakubwa kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuungana na familia kwenye dua hiyo ambayo ipo kwenye mchakato wa kufanywa kuwa siku maalum yenye jina la “King Majuto Day”.

King Majuto amezikwa kijijini kwake Kiruku  kilichopo Kata ya Mabokweni zaidi ya kilomita 20 umbali wa saa moja kasoro kutoka Tanga Mjini.  

Chanzo: www.tanzaniaweb.live