Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani nchini Naibu Kamishna wa Polisi DCP Ramadhan Ng’anzi amesema polisi inajipanga kuanza kukagua magari binasi yanayofanya safari zake nyakati za usiku ili kuzuia visa vya ajali ambavyo vimekuwa vikitokea nchini.
Amesema kwa sasa polisi wanaendesha operesheni ya kukagua magari ya abiria na mizigo usiku kubaini makosa na uzembe unaoweza hatarisha uhai wa watumiaji wa barabara na madereva hao.
Katika operesheni iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika maeneo ya Arumeru mkoani Arusha, askari wa kikosi cha usalama barabarani wamekagua kiwango cha ulevi mwilini kwa madereva, alama za usalama, kiwango cha abiria ndani ya basi na mwendokasi wa magari ya abiria.