Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazawa wajitosa upanuzi TGC

Naibu Waziri Wa Madini Dk Kiruswa.jpeg Naibu Waziri wa Madini, Dk. Stephen Kiruswa.

Tue, 2 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesaini mkataba wa bilioni 33.4 na kampuni mbili za wazawa kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Gemolojia Tanzania (TGC) kilichopo mkoani Arusha kitakachotumika kutoa mafunzo ya uongezaji thamani madini nchini.

Kampuni hizo, Lumocons na Skyward za Kitanzania ziliingia mkataba huo na Wizara ya Madini juzi kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa jengo la ghorofa nane la kituo hicho kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Akizungumza baada ya hafla ya utiaji saini jijini hapa, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Stephen Kiruswa, alisema mradi huo unalenga kupanua kituo hicho ili kutoa mafunzo ya uongezaji thamani madini.

Kwa mujibu wa Kiruswa, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeamua kuimarisha utoaji wa mafunzo katika kituo hicho kwa kupanua miundombinu, kuzalisha wataalamu wengi wa uongezaji thamani madini ya vito na madini.

“Serikali ya awamu ya sita imetoa Shilingi bilioni 33.4, shughuli za ujenzi zitaanza wakati wowote baada ya kusainiwa makubaliano leo (jana),” alisema.

Naibu Waziri huyo, alisema mradi huo ukikamilika utakiwezesha kituo hicho kutoa mafunzo kwa kiwango cha kimataifa na madini nchini yaliyochakatwa kupata soko la ndani na nje.

Alisema lengo la serikali kuanzisha kituo hicho ni kutekeleza Sera ya Madini ya Mwaka 1997 na kuongeza thamani ya madini nchini kwa kutoa mafunzo ya kuchonga miamba.

Kiruswa, alisema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika uchimbaji madini na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji nchini.

Alisema hatua zilizochukuliwa zimewezesha kuongezeka utafiti wa madini, uchimbaji madini, thamani ya madini na biashara zake, fursa za ajira na biashara kwa wananchi.

Akizungumzia kuhusu changamoto zilizopo katika sekta ya madini, alisema serikali inaendelea kutafuta wafadhili ili kupata mitaji kwa ajili ya uanzishaji wa viwanda vya kuchakata madini na maabara.

Mkurugenzi wa Lumocons’, Andrew Shirima akizungumza kwa niaba ya kampuni hizo, aliishukuru serikali kwa kuwa na imani na kampuni za ndani ya nchini.

Shirima, alisema mradi huo utachochea ushindani miongoni mwa kampuni za ndani kutafuta zabuni kubwa za serikali.

"Kwa niaba ya washirika wetu wa utekelezaji, tunaahidi kutekeleza mradi kwa wakati na kwa weledi kama inavyotarajiwa na serikali," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live