Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa pareto Mbeya walia na vishoka, wahofia kupoteza soko

Paretoooooooooo Wakulima wa pareto mkoani Mbeya wakivuna zao hilo

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Wakati msimu wa zao pareto ukianza, wakulima katika Wilaya ya Mbeya wameonyesha hofu ya kupoteza soko kufuatia utitiri wa kampuni bubu zinazonunua zao hilo majumbani.

Pareto ni miongoni mwa mazao makubwa ya biashara yanayolimwa katika baadhi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hususani Mbeya na Songwe ambapo kwa mwaka inazalisha zaidi ya tani 2,500.

Wakizungumza na Mwananchi leo Julai 21, 2024, wakulima katika Wilaya ya Mbeya wamesema kumeibuka kampuni nyingi zinazojihusisha na ununuzi wa zao hilo bila utaratibu.

Mkazi wa kijiji cha Muungano, Michael Mbwelu amesema, “ununuzi wa zao hilo usiozingatia utaratibu unaweza kuathiri soko la zao hili.”

Amesema pamoja na kwamba bei yao ni sawa na kampuni nyingine zilizozoeleka, lakini kilio chao ni namna wanavyonunua hadi maua mabichi, jambo linaloweza kuwaondoa katika soko la ushindani. “Pareto ndilo zao letu la urithi lililotulea na kutuendeshea maisha yetu, tunasomesha na kutegemea zaidi zao hili, lakini kwa namna kampuni zinazokuja kipindi cha msimu huu, tunashangaa sana utaratibu wanaoutumia,” amesema Mbwelu.

Sofia Aron, mkazi wa Kata ya Maendeleo, amesema mbali na utitiri wa kampuni hizo wapo pia vishoka wanaopita nyumba kwa nyumba kununua zao hilo likiwa bado halijawa tayari kuingizwa sokoni.

Ameiomba Serikali kuingilia kati kunusuru uhai wa pareto ili mkulima anufaike na kilimo hicho.

“Hatujui ni madalali wametumwa na nani, kibaya ni kwamba wananunua pareto isiyokomaa, wanabeba kila kitu, wanapita nyumba kwa nyumba.” “Tunaiomba Serikali iingilie kati kutunusuru sisi na zao letu,” amesema Sofia.

Mkulima mwingine, Trifonia Laurent amesema kwa sasa bei ya zao hilo ni Sh3,500 kwa kilo, lakini wanalipwa nyongeza na baadhi ya kampuni. Ameitaka Serikali ichukue hatua na kuweka utaratibu mzuri kwa wakulima na wanunuzi ili kuwepo usawa pande zote.

“Tunatumia gharama kubwa kuandaa mashamba hadi kupatikana mazao haya, inapotokea ubabaishaji katika manunuzi tunaoathirika na kuumia ni sisi wakulima, Serikali ituangalie,” amesema Trifonia.

Mmoja wa maofisa pareto (PCT), mikoa ya Mbeya na Songwe, Mussa Sitta amekiri kuwepo kwa kero hiyo akieleza kuwa tayari wamewasilisha taarifa katika Bodi ya Pareto nchini na wanasubiri hatua zaidi.

“Tunahitaji ubora wa zao hili, wakulima wajitahidi kuanika katika maeneo mazuri na PCT inatoa mbegu bure na bei imekuwa inapanda kila msimu, daraja la kati na juu,” amesema na kuongeza:

“Ili kutengeneza Taifa bora katika zao hilo, zimeanzishwa klabu maalumu kwa shule za msingi na sekondari ambapo wanafunzi wanapewa hadi mitihani na wanaofaulu wanapata zawadi na zaidi ya Sh20 milioni zimetengwa kwa mwaka huu,” amesema Sitta.

Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu jambo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema tayari wamepiga marufuku mkulima yeyote kuuzia mazao yake nyumbani, kwani vipo vituo vilivyotengwa rasmi kwa ajili ya biashara hiyo.

Amesema Serikali imefika maeneo ya wakulima na kutoa elimu na maofisa kilimo akieleza kuwa watachukua hatua za haraka kwa wale wote watakaobainika kununua pareto kinyume na utaratibu.

“Tunapata kero nyingi katika zao hili, lakini mimi mwenyewe nimeshafika kwa wakulima kutoa elimu na hivi sasa msimu umeanza, natarajia kurudi tena kutoa maelekezo, tunachoomba ni ushirikiano kwa wadau watupe taarifa za hao vishoka na kampuni bubu zinazofanya shughuli nje ya utaratibu ili tuwachukulie hatua.”

“Kampuni zinazotambulika zenye leseni kutoka halmashauri ni tisa, iwapo kuna ongezeko au ununuzi wa maua mabichi sina taarifa, maana yake baadhi ya wananchi wanahusika na hatutakubali kuharibu soko na ubora wa zao hili,” amesema Malisa.

Chanzo: Mwananchi