Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wapendekeza bandari ya kupokea gesi

Gesi Asilia Visima (600 X 383) Wadau wapendekeza bandari ya kupokea gesi

Tue, 10 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ili kupunguza gharama za bei ya gesi ya kupikia nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Gesi za Mitungi Tanzania (TZLPGA), Amos Jackson amependekeza bandari ya pekee, sambamba na miundombinu ya kupokea gesi hiyo.

Akifafanua amesema kwa kuwa gesi ya mitungi haizalishwi nchini inaagizwa basi kunapaswa kuwe na bandari ya pekee ya kupokelea gesi ambapo ikiagizwa kwa wingi itapunguza gharama za usafirishaji.

Jackson amesema hayo leo Jumanne, Septemba 10, 2024 wakati Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Jumuiya ya Watoa Huduma za Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Gesi za Mitungi Tanzania (TZLPGA), zikitia saini mkataba wa kuandaa Kongamano la nishati safi la 'Energy Connect 2024.

"Tunajua Serikali inaendelea kulifanyika kazi kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania na tunaendelea kufanya kazi kwa karibu. Pia, tunahitaji maghala ya kupokea gesi hiyo, wanachama wetu wanaendelea na ujenzi.

"Kwa sasa tunapokea tani 15,000 za gesi sawa na kilo 15 milioni kwa wakati mmoja sawa na matumizi yetu ya gesi kwa mwezi.

"Bandari yetu kwa sasa inaweza kupokea tani 5 milioni kumbe tunaweza kuleta meli moja tu kwa mwezi ya tani 15 milioni ikamwaga gesi tukasubiri mwezi mwingine… tunapunguza gharama za usafirishaji," amefafanua.

Aidha amesema kwa kutumia teknolojia za kulipia gesi kama Luku basi itawawezesha watu wa hali ya chini kumudu bei ya gesi.

Katika mkutano huo, Serikali imewaomba wauzaji na wasambazaji wa gesi ya kupikia kupitia mitungi kuendeleza jitihada zao ili kusaidia kukuza idadi ya watu wanaotumia nishati safi nchini.

Hilo limesemwa na Kamishina wa umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Innocent Luoga kwamba ili kufanikisha hilo ni vyema wauzaji na wasambazaji kuhakikisha jitihada za usambazaji gesi zinaenda sambamba na uhakika wa upatikanaji wake na bei.

“Sisi kama Serikali tupo tayari kushirikiana na sekta binafsi na umma kuhamasisha na kuwezesha miundombinu, lakini tunawahitaji wadau kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa sababu unaweza kutoa mitungi sehemu mbalimbali lakini ikawa haipatikani na bei yake iwe ambayo watu wanaweza kumudu,” amesema Luoga.

Amesema kama Serikali inaendelea kuwaomba kuhakikisha gesi inapatikana na kufika kila sehemu ikiwa na bei rahisi na miundombinu ya gesi inakuwepo kila sehemu.

“Isijekuwa tumesambaza mitungi nchi nzima lakini kuna wakati tutashindwa kujaza gesi na sisi tuko tayari kuwaunga mkono na kufanya kazi na sekta binafsi,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wadau wengine kushirikiana na Serikali katika kufanya kampeni za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari na nishati za kuni na mkaa.

Amesema Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na sekta binafsi na wamekuwa wakishiriki katika makongamano yote yanayoandaliwa.

“Hili linaonyesha dhahiri tunaunga mkono juhudi zinazofanywa na sekta binafsi hasa katika suala la nishati ya kupikia, wote tunafahamu kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiyo kinara katika eneo hili si Afrika tu dunaini kote,” amesema Luoga.

"Pia, elimu itolewe watu watumie nishati safi na nitoe rai kwa waandishi wa habari waweze kuandika kila siku umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live