Dar es Salaam. Watalii 64 wamewasili leo Jumamosi Oktoba 12, 2019 nchini Tanzania kwa kutumia Reli ya Tazara kwa lengo la kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.
Watalii hao wametokea Afrika Kusini wakitumia treni ya kifahari ya kampuni ya Rovos Rail ya nchini humo wakitumia siku 15.
Wakiwa na bashasha na hamasa kubwa watalii hao walishuka kwenye treni na kuanza kusakata muziki uliokuwa ukipigwa na bendi ya polisi.
Watalii hao walieleza kuvutiwa na hali ya hewa ya Tanzania na shauku kubwa ya kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo mbuga ya Serengeti, mapambo ya Bagamoyo na Zanzibar.
“Nimevutiwa na hali ya hewa na ukarimu wa Watanzania natamani zaidi kufika Zanzibar nimekuwa nikisoma na kuangalia picha za visiwa hivyo kwa muda mrefu,” amesema John Macmillian.
Ofisa uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Agustina Makoye amesema ujio wa treni hiyo una tija kubwa kwa sekta ya utalii nchini.
Pia Soma
- Mama aeleza gazeti la Mwananchi lilivyomrejesha mwanaye shule
- Simu za mkononi zinavyosaidia ukuaji wa biashara ndogo na za kati (SMEs) -nchini
- Majaliwa ajiandikisha kupiga kura, awaonya wapotoshaji