Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Wataalam wa benki kujadili maadili utoaji wa huduma za fedha

Video Archive
Fri, 9 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa mkutano wa Afrika Mashariki utakaofanyika wiki ijayo utajadili maadili katika utoaji wa huduma za kifedha kupitia mifumo ya kidigitali kutokana na mifumo hiyo kuenea kwa haraka.

Mkutano huo wa wataalam wa benki utakaofanyika jijini Arusha kwa siku tano utawakutanisha washiriki wapatao 100 kutoka nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki.

Watajadili  mwenendo na matukio ya kiteknolojia ambayo yanaathiri huduma za kifedha kama vile benki, mitandao ya simu na bima.

Huu ni mkutano wa 19 katika mfululizo wa mikutano ambayo huandaliwa na taasisi za wataalam wa benki za Tanzania, Kenya na Uganda.

Kumekuwepo na uvumbuzi wa kila mara wa mifumo ya kiteknolojia kama matumizi ya mitandao ya simu ambayo hurahisisha utoaji huduma na kuongeza ufanisi wa benki na taasisi nyingine za fedha.

Hata hivyo, uvumbuzi huo huambatana na athari kama vile wizi wa kimtandao na baadhi ya mifumo kufeli.

Pia Soma

“Tanzania ni moja ya nchi ambazo zinajivunia kuwa na mabadiliko ya kidigitali na Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikifanya kazi ya kuhakikisha usalama wa miamala. Safari hii tunaangazia zaidi maadili katika mifumo hii na utoaji wa huduma za kifedha kwa ujumla,” amesema mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya wataalam wa benki nchini (TIOB),  Patrick Mususa.

“Kuna mifumo mingi sana na mingine hutumia roboti lakini swali ni kwamba mifumo hii imefundishwa maadili? Inazingatia misingi ya utoaji huduma.

Mada zingine zitakuwepo lakini karibu asilimia 70 ya majadiliano yatahusu maadili katika mifumo ya kidigitali.

“Tunao watoa mada wapatao 12 ambao ni wataalam kutoka benki, kampuni za simu, bima na taasisi za elimu ambao watatoa mawazo yao kuhusu mifumo ya kidigitali. Tunatarajia washiriki watajifunza mengi na kufurahia mkutano mzima,” amesema mkurugenzi wa fedha wa TIOB, Damas Mugashe.

Chanzo: mwananchi.co.tz