Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: TRA yataja siri ya kuvunja rekodi makusanyo Septemba

Video Archive
Thu, 3 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imevunja rekodi ya makusanyo mwezi Septemba baada ya kuimarisha mifumo yake ya ukusanyaji kodi nchini.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema ili kufikia malengo yao waliongeza usimamizi wa mashine za risiti za kieletroniki (EFD) na kuhakikisha magari yote ya mizigo yanayotoka Dar es Salaam yanakaguliwa risiti za mizigo na gharama za usafirishaji.

Alisema mamlaka hiyo pia imeweka vituo maeneo ya Msata, Mkuranga na Morogoro pamoja na kuimarisha usimamizi wa mtaa kwa mtaa.

“Pia tumefanya uhamasishaji mkubwa kwa kutumia programu za televisheni, redio, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi kwa walipakodi,” alisema.

Akifafanua zaidi, Kayombo alisema TRA pia imejiwekea mikakati kabambe kuhakikisha wanavuka malengo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa serikali na sekta binafsi

“Tumefanikiwa kuongeza ufanisi wa makusanyo kwa kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kusimamia kikamilifu sheria za kodi, msisitizo wa matumizi ya EFD pamoja na kuweka mazingira rafiki ya ulipaji kodi,” alisema.

Pia Soma

Advertisement
Wakati huohuo, kamishna mkuu wa mamlaka hiyo, Profesa Edwin Mhede akifafanua kuhusu mafanikio ya ukusanyaji wa mapato alisema wamekusanya mapato ya jumla ya Sh1.767 trilioni Septemba mwaka huu na kuweka rekodi ya miaka 23 iliyopita.

Alisema makusanyo hayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 97.20 ya lengo la kiasi cha Sh1.817 trilioni katika kipindi hicho.

“Haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa TRA, ikilinganishwa na makusanyo ya mwezi Septemba 2018, makusanyo ya kipindi hichohicho mwaka huu yamekuwa kwa wastani wa asilimia 29.18.

Alisema ufanisi wa Septemba 2019 ni muendelezo wa ongezeko la makusanyo ya mwaka wa fedha wa 2019/20 ulioanza Julai.

Alisema hatua hiyo inafuatia kipindi cha Julai na Agosti mwaka huu walipofanikiwa kukusanya kiasi cha Sh1.256 trilioni, sawa na asilimia 91.92 ya lengo la kukusanya kiasi cha Sh1.367 trilioni na Sh1.336 trilioni sawa na asilimia 94.05 ya lengo la kukusanya Sh1.409 trilioni.

Mhede alisema makusanyo hayo yanaashiria kuwa walipa kodi na Watanzania wengi wameanza kukubali wito wa Serikali wa kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Itakumbukwa pia kuwa kuanzia Agosti Mosi, TRA ilianza kutumia mfumo wa stempu za kielektroniki (ETS) katika bidhaa za vinywaji baridi kama soda na vinginevyo visivyo na kilevi katika kukusanya mapato.

Hiyo ilikuwa ni awamu ya pili ya kutumika kwa mfumo huo unaosimamiwa na kampuni ya Uswisi ya Societe Indusrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (Sicpa).

Awamu ya kwanza ilianza Januari 15 na ilikuwa ni kwa vinywaji aina ya bia, mvinyo na pombe kali.

Julai 24, Profesa Mhede alitoa taarifa kwa umma ikieleza kuwa bidhaa zote mpya zilizotajwa katika awamu hiyo ya pili zinazozalishwa nchini na zinazoagizwa kutoka nje mpaka Januari 31, 2020 zinatakiwa kuwa na stempu hiyo.

“Wazalishaji na waagizaji wa bidhaa zilizotajwa wanatakiwa kubainisha kiasi cha vinywaji walivyonavyo ambavyo tayari vimezalishwa (ambavyo vinaruhusiwa kuingia sokoni bila mfumo wa ETS) kupitia fomu maalumu inayopatikana katika tovuti ya mamlaka hiyo kabla ya Agosti Mosi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mhede aliwashukuru walipa kodi wote kwa ushirikiano wao ambao wamekuwa wakiuonyesha kufanikisha utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ETS.

Juni, Kayombo aliliambia Mwananchi kuwa takwimu zinaonyesha kuna ongezeko la ukusanyaji wa mapato kutokana na awamu ya kwanza ya mfumo huo.

“Tuna imani mfumo huu utaongeza mapato, kwa awamu ya kwanza tu, tumefanikiwa kuongeza mapato ya ushuru wa forodha kutoka Sh24 bilioni kwa mwezi Januari hadi Sh28 bilioni Aprili,” alisema mpaka wakati huo mashine 44 za ETS zikiwa zimefungwa katika viwanda mbalimbali

“Mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa hesabu halisi za uzalishaji na malipo ya ushuru wa forodha bila kuingiliwa na mtu, tuliwiwa kufanya kazi na Sicpa baada ya kuona mafanikio ya mfumo huu katika nchi za Kenya, Morocco, Uganda, Malaysia, Brazil, Uturuki na Albana,” alisema Kayombo.

Alisema sasa TRA inakuwa na uwezo wa kujua kiwango halisi kinachozalishwa na punde watazindua programu ya simu ambayo itamuwezesha mteja kujua kama bidhaa hiyo ina stempu ya TRA.

“TRA inawashukuru walipakodi wote waliochangia makusanyo hayo kwa kulipa kodi zao kwa hiari, pia tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuisaidia TRA katika kutekeleza majukumu yake ya kukusanya na kuhesabu mapato ya Serikali,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz