Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: TRA yakaribisha majadiliano ulipaji kodi

Video Archive
Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewashauri walipakodi waliofungua mashauri kupinga makadirio ya kodi katika Bodi ya Rufaa za Kodi (Trab), kuyaondoa ili kutoa nafasi ya majadiliano kwa faida ya pande zote.

TRA imetoa wito huo jana ikitoa taarifa ya makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2017/18 inayoonyesha imeshindwa kufikia lengo ililojiwekea kwa kipindi hicho, lakini imeongeza makusanyo kwa asilimia 7.6 kulinganisha na mwaka 2016/17.

“Tunatoa wito kwa wale wenye pingamizi za kodi ambazo zimewasilishwa ofisini kwetu au katika Bodi ya Rufaa za Kodi (Trab) waziondoe kisha waje tuzungumze tuone namna wanavyoweza kulipa,” alisema mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo.

Wakili wa kujitegemea, Edmund Mwasaga alisema wazo la TRA ni zuri akishauri mamlaka itoe hakikisho kwa walipakodi watakaoamua kuondoa mashauri Trab kuwa haki yao ya kuendelea na kesi italindwa hata ikitokea hawatafikia muafaka kwenye meza ya mazungumzo.

“Wazo la TRA ni zuri lakini je, kama hamtafikia makubaliano wakati kesi umeshaiondoa kwenye baraza la kodi kuna namna ya kurudi tena au unakuwa umepoteza moja kwa moja?” alihoji wakili Mwasaga ambaye pia ni meneja mwandamizi wa Masuala ya Sheria wa Benki ya Exim.

Aliishauri TRA kuandaa utaratibu kwa kushauriana na Bodi ya Rufaa za Kodi ili kuzisimamisha kwa muda kesi zilizowasilishwa kwenye meza ya mazungumzo na kama TRA itafikia muafaka na mlalamikaji muafaka usajiliwe ili kesi iondolewe barazani.

Hatua ya TRA kuwaalika walipakodi kumaliza migogoro mezani inakuja siku chache baada ya mamlaka hiyo kutangaza msamaha wa riba na adhabu ya madeni ya nyuma ya kodi kwa asilimia hadi mia moja ili kutoa unafuu kwa walipakodi wenye malimbikizo kulipa kodi ya msingi pekee.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, alisema msamaha huo ni matokeo ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais John Magufuli katika Mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara (TNBC) uliofanyika Ikulu, Machi.

Katika mkutano huo, wafanyabiashara walilalamikia kuwapo kwa malimbikizo makubwa ya madeni ya kodi za nyuma yakijumuisha riba na adhabu.

Jana, Kayombo aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika bajeti kuu ya mwaka wa fedha 2017/18, TRA ililenga kukusanya Sh17.1 trilioni lakini mpaka mwaka unaisha fedha zilizokusanywa ni Sh15.5 trilioni, ikiwa ni tofauti ya Sh1.6 trilioni.

Katika taarifa ya makusanyo ya mwaka mzima iliyotolewa jana, Desemba 2017 ndiyo uliongoza kwa makusanyo ya Sh1.63 trilioni, huku Aprili ikikusanya kiasi kidogo zaidi cha Sh1.07 trilioni.

Alisema mafanikio hayo yametokana na kampeni ya uandikishaji walipakodi na elimu ya kodi kuendelea kueleweka kwa wananchi.

Alisema wamejipanga kukusanya malimbikizo ya kodi na madeni ili kufikia malengo ya ukusanyaji kodi.

Chanzo: mwananchi.co.tz