Dar es Salaam. Waziri wa Elimu nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako ameeleza namna Serikali ilivyowekeza katika ya elimu kuhakikisha inafikia azma ya kuwa na wananchi walioelimika, wenye maarifa, stadi za maisha na mtazamo chanya.
Ameeleza hayo leo Alhamisi Septemba 19, 2019 katika mjadala wa vijana na elimu katika jukwaa maalum maarufu kama Mwananchi Jukwaa la Fikra linalofanyika katika ukumbi wa Kisenga, jijini Dar es Salaam.
Profesa Ndalichako aliyeanza kwa kuipongeza kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) kwa kuandaa jukwaa hilo leo ikiwa ni mara ya tano, amesema linaisaidia Serikali kusikia masuala ya wananchi.
Amebainisha kuwa kuanzia Januari 2016 hadi Agosti, 2019 Serikali imetumia zaidi ya Sh900 bilioni kugharamia elimu bure ambayo imekuwa na mwamko mkubwa na kusababisha changamoto ya vyumba vya madarasa.
Amesema Serikali imejaribu kupambana na changamoto hiyo, imeshatumia zaidi ya Sh300 bilioni kuboresha miundombinu ikiwemo shule mbalimbali zikiwemo kongwe 62 kati ya 88 zilizopo.
“Tumejenga madarasa 2876, mabweni 533, nyumba za walimu na miundombinu mingine ya shule. Tangu Serikali hii iingie madarakani tumeweza kutoa mikopo ya zaidi ya Sh1 trilioni kwa wanafunzi wa elimu ya juu,” amesema Profesa Ndalichako.
Habari zinazohusiana na hii
- VIDEO: Mamia wajitokeza kushiriki Jukwaa la Fikra la Mwananchi
- MWANANCHI JUKWAA LA FIKRA: KUWAWEZSHA VIJANA KUWA NA MAARIFA NA UJUZI MAHUSUSI
- VIDEO: Profesa Kusiluka achambua wanaobeza wahitimu