Dodoma. Licha ya mfumuko wa bei kutajwa kuwa umeongezeka kutoka asilimia 3.0 Novemba 208 na kufikia asilimia 3.8 Novemba 2019, Serikali ya Tanzania imesema bado upo ndani ya lengo.
Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Philipo Mpango ametoa kauli hiyo leo Jumanne Desemba 31, 2019 jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya uchumi wa taifa katika mwaka 2019 na tathimini ya awali ya utekelezaji wa bajeti kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2019/20.
Waziri Mpango ametaja lengo la asilimia 5.0 ambacho ni kiwango kilicho chini ya lengo la nchi za Jumuiya za Afrika Mashariki la asilimia 8.0.
Hata hivyo, Waziri Mpango amesema mfumuko wa bei uliongezeka kufikia wastani wa asilimia 6.7 katika Novemba 2019 ikilinganishwa ana asilimia 2.0 katika kipindi kama hicho 2018 huku zikitajwa sababu za kupaisha mfumuko ni changamoto za usafirishaji, miundombinu ya masoko, maghara na ugavi pamoja na uhaba wa vyakula kwa baadhi ya nchi jirani.
“Hata hivyo, ongezeko hili la bei za vyakula linategemewa kuwa la muda mfupi, kwani bado yetu ina akiba ya chakula cha kutosha ya tani 53,000 lakini napenda kutoa wito kwa wananchi hususani wakati huu ambao mvua zinanyesha sehemu mbalimbali za nchi,” amesema Waziri Mpango.
Waziri Mpango amesema katika kipindi hicho thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea tulivu hadi Novemba 2019 ambapo dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Sh2,291 ikilinganishwa na Sh2,276.
Amesema mwenendo wa sekta ya kibenki imeendelea imara, salama na yenye kutengeneza faida ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha zaidi ya kiwango kinachotakiwa kisheria.
Kwa mujibu wa Waziri Mpango uwiano wa mitaji ya mabenki ukilinganisha na rasilimali zao ulikuwa asilimia 16.23 katika kipindi cha Juni 2019 ikiwa ni juu ya kiwango kinachohitaji kisheria cha asilimia 10.0.
Hata hivyo, amelia na riba kubwa wanazotozwa wananchi wanapokwenda kukopa katika taasisi ndogo ndogo za fedha akisema lazima jambo hilo liangaliwe na kuwekewa ukomo maalumu vinginevyo hali itakuwa mbaya zaidi.