Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Magufuli aeleza miaka mitatu ya mvutano Serikali, kampuni ya Barrick

Video Archive
Fri, 24 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amezipongeza timu za majadiliano kati ya Serikali na kampuni ya madini ya Barrick Gold, “haikuwa rahisi  kufikia makubaliano yaliyoanza mwaka 2017.”

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 24, 2020 Ikulu Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kamati ya madini ya Barrick.

Baada ya mgogoro uliodumu tangu mwaka 2017, Kampuni ya Barrick na Serikali ziliunda kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.

Kwenye kampuni hiyo mpya, Barrick itamiliki asilimia 84 ya hisa zote huku Serikali ikiwa na asilimia 16. Utaratibu huo ni utekelezaji wa sheria mpya ya madini iliyopitishwa mwaka 2017.

Mgogoro kati ya Serikali na kampuni ya Acacia iliyokuwa inasimamia migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulanhulu ulianza mwaka 2017 na Rais Magufuli akaunda tume ya kuchunguza mwenendo wa biashara ya madini.

Tume hiyo ilibaini ukiukwaji wa sheria, utaratibu na kanuni zilizopo hivyo kuikosesha Serikali mapato inayostahili. Kutokana na hilo, Serikali iliipiga faini ya Dola 190 bilioni jambo lililosababisha kuanza kwa mazungumzo baina ya pande hizo mbili.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Kwenye mazungumzo hayo, Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick iliwekwa pembeni na majadiliano yakafanywa na Barrick, mwisho wa siku, Acacia imefutwa sokoni na badala yake, Twiga itachukua nafasi yake.

Katika maelezo yake ya leo, Magufuli amesema makubaliano hayo yalimpa wakati mgumu Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi aliyekuwa akiongoza timu ya Serikali.

“Kabudi mengine hakuyasema, jinsi alivyokuwa anapata misukosuko. Nilikuwa nampigia simu saa saba usiku, asipopokea namba zake zote napiga nyingine. Akipokea ni matusi, ananizidi umri lakini ana uvumilivu. Nakupongeza Profesa,” amesema Rais Magufuli.

Pia, amewapongeza wataalamu walioshiriki kwenye majadiliano hayo, huku akiihakikishia kampuni ya Barrick Gold kuwa Tanzania ni sehemu sahihi ya uwekezaji.

“Ilikuwa tutafute wanasheria na washauri tuwalipe, tulisema sisi hatujitaji wanasheria tunahitaji wazalendo wazungumze na wazalendo wenzao wa Barrick na ndiyo maana tumefikia hatua hii.”  

“Wafikishieni salamu wenzenu wa Barrick mwaambe kuwa Tanzania  ni sehemu bora ya kuwekeza,” amesema Magufuli.

Amebainisha kuwa mchakato huo haukuwa rahisi akifananisha kampuni ya Barrick  na ng’ombe anayegombana na sungura kutokana na utajiri wake.

“Unapoingia kwenye mchezo wa kushindana kati ya ng’ombe na sungura, huyu ni mzito na huyu ni mwepesi,” amesema Magufuli, akibainisha kuwa Tanzania ina madini, kampuni hiyo inayachimba hivyo lazima kugawana sawa.

Chanzo: mwananchi.co.tz