Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Madereva wachekelea, wachuuzi walia kuanza kwa barabara za juu Tazara

Video Archive
Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hatimaye barabara za juu (flyovers) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela, Tazara jijini Dar es Salaam zimeanza kutumika jana baada ya ujenzi wa miezi mitano.

Ujenzi wa barabara hizo ulizinduliwa Aprili 16 na Rais John Magufuli ambapo mradi huo ulijengwa kwa ushirikiano na Serikali ya Japan.

Katika mradi huo Japan kupitia shirika lake la ushirikiano wa kimataifa (Jica), waliotoa Sh93.4 bilioni huku Tanzania ikitoa Sh8.3 bilioni.

Katika siku ya kwanza ya kutumia barabara hizo jana, watumiaji hasa madereva walipongeza ujenzi huo wakisema utapunguza foleni katika makutano ya Tazara.

Hata hivyo, wachuuzi wanaouza bidhaa katika barabara za Mandela na Nyerere, eneo la Tazara walidai foleni ilikuwa ikiwasaidia kufanya biashara na sasa watapata wakati mgumu kuuza vitu vyao.

Dereva Wansislaus Shoo alisema kabla ya kufunguliwa kwa barabara hiyo alikuwa akitumia wastani wa saa mbili kutoka eneo la makutano ya barabara hizo kwenda kokote jijini Dar es Salaam, jambo lililoathiri shughuli zake.

Kondakta wa daladala inayotoka Vigunguti kwenda Temeke aliyejitambulisha kwa jina moja la Said, alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kuongeza idadi ya safari wanazofanya kila siku hivyo kuwaongezea kipato.

“Foleni ya eneo hili (Tazara) ilituumiza watu wa biashara ya usafiri, ilinifanya nizunguke safari nne hadi tano tu kwa siku, lakini kwa dakika zilizopungua itanisaidia kuzunguka safari sita hadi saba. Kiukweli nashukuru sana kwa ujenzi wa barabara hii,” alisema kondakta huyo huku akionyesha tabasamu.

Wachuuzi walia

Mchuuzi wa mihogo na karanga katika makutano hayo, Neema Chaula alisema kabla ya kuanza kutumika kwa barabara hizo alikuwa akiuza kati ya Sh4,000 hadi Sh4500 kwa siku, lakini hadi saa 8:00 mchana jana alikuwa ameuza Sh500 kutokana na kupungua kwa foleni.

“Foleni hamna sasa utauza nini na foleni ndiyo ilikuwa biashara kwetu, magari yamepungua mno. Sisemi ni vibaya kujenga barabara hizo, lakini inabidi kutafuta maeneo mengine (ya biashara zetu),” alisema Neema.

Innocent Joel anayeuza maji eneo hilo alisema biashara imekuwa ngumu kwake. “Biashara imekuwa ngumu, inabidi tuangalie maeneo mengine ya kufanyia lakini hapa leo hali siyo nzuri,” alisema.

Awali, wakati wa uzinduzi wa mradi huo, mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Patrick Mfugale alisema kukamilika kwake kutapunguza muda wa kukaa kwenye foleni kwa asilimia 80 kwenye makutano hayo.

Hata hivyo, Tanroads jana hawakutaka kuzungumzia suala hilo wakidai hadi barabara hizo zitakapozinduliwa.

Agosti 29, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea ujenzi wa barabara hizo na kueleza kuwa umekamilika kwa asilimia 98. Pia alisema wakati wowote mwezi ujao Rais Magufuli atazizindua.

Chanzo: mwananchi.co.tz