Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Alishokisema mbunge Shabiby kuhusu mashine za EFD, usafirishaji

Video Archive
Wed, 19 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby ameitaka Serikali ya Tanzania kuzichunguza mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD) kwa maelezo kuwa nyingi ni mbovu.

Pia, amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kufuatilia sababu za Watanzania kusajili magari yao nchi jirani licha kuwa yanapitia Tanzania.

Shabiby ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 18, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

"Mashine za EFD zimekuwa kero, sijajua tatizo ni kampuni zilizopewa tenda au la. Kila siku ni mbovu sasa zimekuwa mtaji kwa watu utaambiwa mashine mbovu nunua nyingine," amesema.

Kuhusu mashine za EFD katika vituo vya mafuta Shabiby amesema, “Ni wizi mtupu na TRA mnajua ila kwa kuwa watendaji wengi kwa sasa ni wapya hamkuwepo wakati mashine hizi zikiletwa. Unanunua mashine kwa dola 3,000 au 5,000 unaifunga kituoni kwa mwaka unalipa Sh1.2 milioni kwa ajili ya fundi harafu Mkoa mzima kuna fundi mmoja.”

“Mashine ikiharibika unatoa ripoti TRA na akija fundi kila pampu anachukua Sh300,000, pia makaratasi yanayotumika ni ya mamilioni.”

Pia Soma

Shabiby amesema kama ni makato kila lita ya mafuta inajulikana wazi kiasi cha fedha anachopata mhusika, kuhoji sababu za fedha hizo kutokatwa kabla mhusika kuchukua mafuta kwenye vituo.

“Kuna watu wa bodaboda wanauza mafuta rejareja mnawadhibiti vipi, sasa EFD inafanya nini? Mimi naweza kuwa na mafuta lakini sipeleki kituoni nashusha shambani au kwenye gereji yangu mtajuaje,” amesema Shabiby.

Kuhusu usajili wa magari, Shabiby amesema siku za hivi karibuni magari mengi ya Watanzania yanasajiliwa katika nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na Zambia na kwamba magari hayo hupitia Tanzania.

“Zile gari zenye namba ya IT nyingi ni za Watanzania na zinapita nchini kwenda katika nchi hizo hapo maana yake kodi yote inakwenda huko.”

“Gari za IT  zinahamia kwenye nchi za jirani tatizo ni nini. Naomba watu wa TRA (Mamlaka ya Mapato) wajaribu kukaa na wafanyabiashara kuona shida ni nini hadi watu wanahama kupeleka kodi kwenye nchi nyingine,” amesema Shabiby.

Chanzo: mwananchi.co.tz