Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uongozi solo la Kariakoo wakanusha ugawaji wa vizimba kinyume na utaratibu

Uongozi Solo La Kariakoo Wakanusha Ugawaji Wa Vizimba Kinyume Na Utaratibu.jpeg Uongozi solo la Kariakoo wakanusha ugawaji wa vizimba kinyume na utaratibu

Fri, 28 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirika la Masoko ya Kariakoo linatoa taarifa kwa umma kwamba kwa sasa hakuna vizimba au maeneo mengine ya biashara yaliyogawiwa au kuuzwa kwenye soko la Kariakoo kama walivyodai baadhi ya wafanyabiashara walionukuliwa na vyombo vya habari hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika hilo Sigsibert K. Valentine, alisema wananchi waepuke vishoka au watu wengine wanaodai kuwa vizimba vinauzwa au kukodishwa kinyume cha taratibu za Serikali.

“Serikali bado haijaanza kupangisha maeneo ya biashara au vizimba kwenye soko la Kariakoo. Wananchi wawe watulivu na taarifa rasmi za upangishaji zitatolewa” alisema Valentine.

Kuhusu zoezi la uhakiki Valentine alifafanua kuwa halilengi kuwapunguza wafanyabiashara bali kuweka kumbukumbu sahihi za wafanyabiashara ili ziwekwe kwenye mfumo wa kidigitali tofauti na ilivyokuwa awali

Kwa sasa Shirika linaendelea kutekeleza mipango ya Serikali ikiwemo kukamilisha ujenzi wa soko jipya na ukarabati wa soko la zamani, kuweka kumbukumbu sahihi za wafanyabiashara waliokuwepo kabla ya ajali ya moto, kuandaa mpangilio mzuri wa biashara na wafanyabiashara (market segmentation) na kuratibu maandalizi ya elimu kwa wafanyabiashara kuhusu mfumo wa TAUSI na Bima.

Shirika linatoa shukrani kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa Shilingi Bilioni 28.03 kutekeleza mradi huu wa kimkakati ambapo nafasi za biashara 3,500 na ajira zaidi ya 4,000 zitapatikana. Mradi unaendelea vizuri ambapo hadi Juni 2024 umefikia asilimia 93 na mkandarasi amelipwa zaidi ya Shilingi Bilioni 20.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live