Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ungana na Mwananchi Communication kujadili Afya Yetu, Mtaji Wetu leo

Video Archive
Thu, 28 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) imezindua Jukwaa la Fikra litakalowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali na wananchi, ili kujadiliana kuhusu mada za kitaifa na kizalendo.

Mjadala wa kwanza unatarajiwa kufanyika leo katika Ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3.00 usiku hadi saa 5 usiku na kurushwa mubashara kupitia vituo vya ITV, Radio One na mitandao yote ya kijamii ya MCL ikiwamo MCL Digital.

Katika mjadala wa kwanza, mada kuu ni ‘Afya Yetu, Mtaji Wetu’ inayolenga kuangalia changamoto zinazotokana na magonjwa yasiyoambukiza nchini (NCD).

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari jana, mkurugenzi mtendaji wa MCL, Francis Nanai alisema mada mbalimbali za kitaifa na kizalendo zitajadiliwa kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa pamoja kuhusu changamoto zinazolikabili Taifa. “Nina furaha kubwa kuwakaribisha nyote kwenye mjadala huu wa kwanza kabisa wa Mwananchi Jukwaa la Fikra tukiangalia magonjwa yasiyoambukiza,” alisema.

Nanai alisema jukwaa hilo linalenga kuwaleta pamoja viongozi wa Serikali, watunga sera, wadau, taasisi za kimataifa na kikanda, watendaji wakuu wa kampuni na mashirika mbalimbali, wanadiplomasia, wataalamu kutoka sekta mbalimbali, wasomi, wanafunzi, waathirika na Watanzania wote wanaolitakia mema Taifa.

Alisisitiza kuwa jukwaa hilo ni la kutafuta suluhisho la pamoja na si kunyoosheana vidole.

Mkurugenzi huyo alisema MCL imeamua kuanza na mada ya magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu ni miongoni mwa magonjwa yanayoipa mzigo mkubwa Serikali na kuathiri idadi kubwa ya Watanzania.

“Tatizo ni kwamba magonjwa haya hata kama hayajakuathiri wewe moja kwa moja, basi yatakuathiri kupitia kwa wale ulio karibu nao kama familia, ndugu, rafiki au kupitia mzigo wa huduma za afya ambao unabebwa na ama Serikali, mwajiri au familia ambazo hulazimika kutumia rasilimali zake kukabiliana na magonjwa haya,” alisema.

Alisema kukiwa na mjadala wa pamoja wa wadau muhimu wa sekta ya afya na hasa wataalamu wa magonjwa yasiyoambukiza, MCL ina imani kuwa jukwaa litatoa fursa ya wao kuwa na majadiliano ya kina wakiwashirikisha Watanzania wengine na kuangalia changamoto na matatizo yaliyopo.

“Muhimu sana ni kupendekeza suluhisho ambalo wanadhani litasaidia kukabiliana na changamoto hizo na upande wa Serikali na watunga sera kuwa tayari kuyachukua mapendekezo na kuyafanyia kazi,” alisema Nanai.

Baada ya mjadala

Nanai alisema baada ya kufanyika mjadala huo, Jukwaa la Fikra litakusanya mrejesho na kuandika ripoti itakayoainisha mapendekezo ya nini kifanyike.

Alisema ripoti hiyo itakabidhiwa kwa wizara husika na wadau wengine kwa ajili ya utekelezaji katika maeneo yanayowahusu. “Siyo kwamba tutaishia kuzungumza pale na kuondoka lakini kama waandaaji tumejipanga kuandika kwa ufupi nini kimezungumzwa, mapendekezo gani yametolewa na tutaandika ripoti na kupeleka wizara husika ili kuona nini kifanyike kutatua tatizo hilo,” alisema Nanai.

Alisema Jukwaa la Fikra ni fursa nzuri na akawaomba Watanzania waishio Dar es Salaam wahudhurie ili kwa pamoja waweze kuzungumzia suala hilo na kupata ufumbuzi.

Nanai alisema kuanzia sasa kila baada ya miezi mitatu Mwananchi Jukwaa la Fikra litakuwa na kitu cha kujadiliana kuhusu matatizo yaliyopo katika nchi na likilenga ufumbuzi kwa kupendekeza serikalini nini kifanyike.

Mkurugenzi huyo aliwataja baadhi ya washirika waliowezesha kufanyika kwa uzinduzi wa jukwaa hilo kuwa ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Shirika la Afya Duniani (WHO) huku akitoa shukrani za pekee kwa ITV/Radio One ambao alisema ndiyo washirika wakuu kwa upande wa habari.

“Tunawashukuru pia wafadhili wetu wakiwemo Mfuko wa Bill & Melinda Gates, Benki ya NMB pamoja na Hotel & Club ya mazoezi ya Colloseum kwa michango yao ya hali na mali katika kufanikisha jukwaa hili,” alisema na kuongeza:

“Nina furaha kubwa kuwakaribisha wote na ni matarajio yangu kuwa mjadala huu utatuwezesha kupata ufumbuzi ambao utalisaidia Taifa katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.”

Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Joyce Mhaville aliishukuru MCL kwa ubunifu ambao alisema kuwa ni wa kisasa zaidi na utawapa wananchi na wadau uwanja mpana wa kujadili matatizo yanayowakabili na kupata suluhisho.

“Kwanza niishukuru MCL kwa kuona umuhimu wetu sisi kama ITV/Radio One kuwepo katika jitihada hizi, lakini pia niwapongeze kwa ubunifu ambao unalenga kuwasaidia Watanzania walio wengi na Taifa hili kwa ujumla. Ninaamini kuwa jukwaa hili litafikia malengo yake kwa maana ya kufikia kile kinachotarajiwa,” alisema Mhavile.

Chanzo: mwananchi.co.tz