Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tembo Nickel yaweka rekodi mpya nchini

Madini Nickel Kabanga Tembo Nickel yaweka rekodi mpya nchini

Wed, 24 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAMPUNI ya Tembo Nickel kupitia kampuni yake mama ya Lifezone Metals imeandika historia hapa nchini kwa mara ya kwanza kwa kuzalisha madini ya nikeli, shaba, na kobalt zilizosafishwa kutoka kwenye Mradi wa Kabanga Nickel ulioko Ngara, Kagera.

Hatua hiyo muhimu imefikiwa wakati wa majaribio yaliyofanywa katika Maabara ya Lifezone ya kisasa ya Simulus kwa kutumia Teknolojia yao ya ubunifu ya Hydromet.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde imesema uzalishaji huo ni wa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu miongo mitano tangu ugunduzi wa madini hayo katika eneo la Kabanga hapa nchini na kwamba mafanikio hayo yanaendana kikamilifu na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza thamani ndani ya nchi.

“Kwa mafanikio haya, Tembo Nickel inaweka msingi imara kwa Kiwanda chake cha Usafishaji Metali Anuai kitakachokuwa Kahama mkoani Shinyanga ambacho kitazalisha madini ya ubora wa juu yaliyopatikana kwa kuzingatia uendelevu hapa hapa Tanzania, ambacho tayari Tume ya Madini wameshatoa Leseni husika na hivyo kupelekea kuanza kwa hatua za awali za ujenzi wake.” Ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa hiyo ni hatua muhimu katika kuifanya Tanzania kuwa kati ya nchi vinara duniani katika uzalishaji wa nikeli ya Daraja la 1 na madini mengine ya kimkakati.

Waziri Mavunde alieleza kwenye taarifa hiyo kuwa Tanzania iko tayari kukumbatia uwekezaji wa kuchimba madini wenye uwajibikaji na ubunifu ambao unaweka kipaumbele uongezaji wa thamani ndani ya nchi na maendeleo endelevu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live