Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA: Hakuna biashara itakayofungwa - VIDEO

Video Archive
Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema hakuna mtu atakayefungiwa biashara yake kwa sababu ya kuchelewa kulipa kodi au malimbikizo ya kodi, na endapo itaonekana kuna ulazima wa kufanya hivyo kibali kitatolewa na kamishna mkuu wa mamlaka hiyo.

Suala la kufunga biashara kwa sababu ya madai ya kodi limekuwa likilalamikiwa na wafanyabiashara wengi pamoja na viongozi wakuu wa Serikali akiwamo Rais John Magufuli na wote wamekuwa wakihoji ni wapi mfanyabiashara atapata fedha anayodaiwa ikiwa biashara yake imefungwa.

Akizungumza jana katika mahojiano maalumu alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam, mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema jambo hilo limesitishwa tangu mwishoni mwa mwa mwaka jana.

Alisema tayari kamishna mkuu wa TRA, Charles Kichere ametoa maelekezo kwa mameneja wao wa mikoa na wilaya. “Malalamiko yalikuwepo mwaka jana tulijitafakari na kuyafanyia kazi, tulikuwa na wakala aliyekuwa anakusanya malimbikizo hayo ya kodi kwa niaba yetu, ndiye alikuwa anafanya hivyo lakini sasa kazi hiyo tulimpa sisi, hivyo hatuna budi kuzikubali hizo lawama lakini jambo hilo sasa halipo,” alisema.

Kayombo ambaye aliambatana na maofisa wengine wa TRA, alisema sasa wafanyabiashara wanafuatwa kistaarabu na kuhimizwa kulipa kodi wanazodaiwa bila kusimamisha biashara zao wala kusababisha usumbufu.

“Sasa hakuna kufunga biashara ya mtu, TRA itazungumza na mfanyabiashara, watakubaliana namna ya kulipa na utaratibu utakaotumika, na endapo mtu atakaidi kulipa kwa makusudi na ikaonekana kuna ulazima wa kumfungia biashara kibali cha kufanya hivyo kitatolewa na kamishna mkuu tu.”

Alisema ili kuendelea kujenga ukaribu wa TRA na wafanyabiashara mameneja wa mikoa na wilaya wameagizwa kukutana na wafanyabiashara kila Alhamisi kuzungumza nao ili kujua changamoto zao na kuelekezana.

Kuhusu suala la TRA kutumia bunduki kudai kodi, alisema siyo utaratibu wa mamlaka hiyo na ili kuepuka vishoka ni muhimu walipakodi wakajua kuwa TRA kabla haijaja kukagua biashara inatoa taarifa kwanza na siku ya ukaguzi, mkaguzi anapaswa kujitambulisha na kutoa kitambulisho.

“Huo siyo utaratibu wetu, hata hivyo bahati mbaya iliyopo ni kwamba hata vyombo au taasisi nyingine zikienda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria zinazowasimamia, watu wanasema ni TRA,” alisema.

Kodi kabla ya biashara

Kayombo alisema TRA imekwishaachana na utaratibu wa kumtaka mfanyabiashara kulipa kodi kabla ya kuanza biashara yenyewe na badala yake, hivi sasa mtu anaweza kulipa baada ya kufanya biashara kwa miezi mitatu.

“Ulipaji wa kodi kwa mwaka tunaugawanya katika robo nne, kabla ya Januari 2018 mfanyabiashara alikuwa anatakiwa kulipia kwanza ndipo afanye biashara, lakini sasa anaruhusiwa kulipa baada ya robo ya kwanza. Hata hivyo mwenye uwezo wa kulipa kabla hazuiliwi,” alisema Kayombo.



Chanzo: mwananchi.co.tz