Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene amegoma kufungua machinjio ya Msalato kutokana na kutoridhishwa na ukarabati uliofanyika.
Oktoba, 2019 Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) liliyafunga machinjio hayo yanayomilikiwa na Jiji la Dodoma na kuwatoza faini ya Sh5 milioni kwa uchafu.
Akizungumza leo Jumatano Januari 22, 2020 baada ya kutembelea machinjio hayo, Simbachawene amesema jengo hilo lililokarabatiwa kwa Sh22 milioni halina viwango vya Serikali.
“Hili si jengo la Serikali ni la mlalahoi anaamua kujenga hivi lakini sio viwango vya Serikali. Sasa nikiuliza hela zilizotumika ni fedha za ajabu..., ninasema silifungui hao ng’ombe mchinjie mikononi haiwezekani jengo la serikali likawa ovyo namna hii,” amesema Simbachawene.
Kutokana na kutoridhika na ukarabati huo, waziri huyo ametoa wiki moja kwa uongozi wa Jiji la Dodoma kufanya marekebisho.