Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shigongo, Mwigulu wavutana Tanzania kurudi Uchumi wa Chini

Shigongo Mwigulu Gdp Shigongo na Mwigulu

Mon, 9 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MVUTANO umeibuka bungeni baina ya Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba kuhusu nchi kuporomoka kwa kiwango cha uchumi wa Taifa kutoka uchumi wa kati hadi uchumi wa chini.

Mvutano huo umeibuka bungeni leo Jumatatu, Mei 9, 2022 baada ya Shigongo kueleza bungeni hapo kuwa taifa limeporomoka kutoka uchumi wa kati hadi uchumi wa chini tofauti na miaka miwili iliyopita.

Mbunge huyo amesema pato la mtu mmoja mmoja limeshuka hadi Dola za Marekani 976 na hivyo kuifanya Tanzania kukosa sifa zinazoifanya nchi kuwa uchumi wa kati.

“Nchi yetu Tanzania miaka miwili iliyopita tulisheherekea tukashangilia kwa pamoja kupanda mpaka uchumi wa kati, GDP ya Taifa ilikuwa, ‘per capita income’ ikaongezeka na hivyo tukasheherekea kwamba nchi yetu inakwenda vizuri.

“Lakini ninavyozungumza na wewe hivi sasa nchi yetu imerudi tulipokuwa, ‘per capita income’ imeshuka hadi Dola za Marekani 976, ina maana tumeporomoka chini kwa sababu yeyote ile iwe covid-19 au yeyote ile ukweli tumeporomoka,” amesema Shigongo.

Wakati akieleza hayo, Waziri mwigulu aliomba kuweka sawa jambo hilo na kueleza kuwa kilichoshuka ni ukuaji wa uchumi (growth rate) na si viwango vya pato la Taifa (level of income).

“Nataka niweke kumbukumbu sawa kwamba hatujarudi tulipokuwa na hii naomba isikike vizuri sana. Tulitoka uchumi wa chini tukaenda uchumi wa kati wa chini hatujawahi kurudi uchumi wa chini tena.

“Tunachozungumza ni ukuaji na si level ya uchumi. Kuna tofauti ya level of income ya nchi na growth rate,” amesema Mwigulu.

Amesema kilichobadilika ni kutoka ukuaji wa asilimia saba na kushuka hadi asilimia nne ya ukuaji wa uchumi “na tangu tushuke tushapanda hadi 4.9.”

Waziri huyo amesema kwa takwimu zinazokamilika za 2021 ukijumlisha wastani wanaenda asilimia tano “na kwa mwaka 2022 tunaenda asilimia 5.2 na hata wenzetu wa Benki ya Dunia juzi walisema huenda tukaenda hata 5.5,” alisema Mwigulu.

Hata hivyo Shigongo hakukubaliana na hoja za Mwigulu ambapo akieleza kuwa kigezo kinachotumika nchi kuwa uchumi wa kati ni kuwa na pato la mtu mmoja mmoja la kati ya Dola za Marekani 3033 hadi 4045 na kwamba Tanzania ilifikia Dola 3080 ndiyo ikafika uchumi wa kati.

Alisema kwa takwimu za sasa pato la mtu mmoja mmoja limefikia Dola za Marekani 976 hivyo ni dhahiri kuwa nchi imerudi uchumi wa chini.

“Ndiyo maana na sema tumerudi kwasababu ‘per capita’ imeshuka, hoja yangu ni kwamba kurudi nyuma sio sababu cha msingi ni kushirikiana na wabunge turudi tulikokuwa uchumi wa kati, na hili litawezekana kwa kuimarisha kilimo kwa kutafuta masoko,” amesema Shigongo.

Shigongo ameomba TANTRADE kupewa fedha za kutosha ili iweze kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo za Tanzania badala ya kuishia kuandaa maonesho ya sabasaba.   Ikukbukwe kuwa, Aprili 5, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi wa dini alisema kwamba; ingawa Tanzania imeondolewa kwenye nchi zenye uchumi wa kati lakini kufikia mwaka 2025 Tanzania itakuwa imefika au imekaribia kurudi uchumi wa kati.

"Tanzania tuliingia uchumi wa kati tukarudishwa, siyo kwa mipango ya mtu, ni mipango ya Mungu. Kwahiyo tupambane kurudi tulipokuwa. Na kwa ninavyoiongoza serikali, natarajia kufikia 2025 tutakuwa tumefika au tunakaribia kurudi uchumi wa kati," alisema Rais Samia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: