Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kujenga ghala kubwa la mpunga Shinyanga

Mpunga.png Serikali kujenga ghala kubwa la mpunga Shinyanga

Fri, 13 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Kilimo, Husein Bashe ametembelea mradi wa umwagiliaji wa Nyida uliopo mkoani Shinyanga chini ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NiRC) na kuelekeza kuwa ndani ya mradi huo lijengwe ghala kubwa la kuhifadhi mpunga.

Waziri Bashe ameelekeza pia ufanyike ujenzi wa kituo cha pamoja cha kununua mpunga na kufungwa mashine na kinu cha kuchakata mchele, sambamba na ujenzi wa barabara ya uhakika yenye urefu wa km 7.5 itakayoungana na barabara kubwa ya lami. Hilo ametaka liwe sambamba na kujengwa kwa mabirika kunyweshea mifugo.

Waziri Bashe amesema hayo katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ukiwemo huo wa Nyida.

Waziri Bashe pia ameelekeza kuongezwa kwa mradi mdogo wa Nyida wenye ukubwa wa hekta zaidi ya 400 na kuagiza skimu hiyo itangazwe hivi karibuni na ujenzi uanze haraka.

Waziri Bashe, amesisitiza kuwa bwawa hilo lenye ujazo mita za ujazo milioni 7 na mfumo wa kutoa maji yanapojaa itasaidia kuepuka maji yanayofurika na kuharibu miundombinu ya barabara.

Amesema ujenzi wa miradi hiyo iliyoanza, kwa upande wa Nyida pekee serikali inatumia fedha za walipa kodi zaidi ya shilingi bilioni 55 sawa na vituo vya afya 100.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NiRC, Raymond Mndolwa, amesema Tume inaendelea na mpango wa kujenga mabwawa, kukarabati skimu za zamani na kuibua maeneo mapya kwa ajili ya kilimo.

“Mkoa wa Shinyanga una jumla ya skimu 14, sikimu nyingi zilijengwa muda mrefu na hivyo sasa ni chakavu na nyingine kutokamilika ikiwemo Ishololo, Mwamashele, na Kahanga,” amesema.

Aidha kwa mwaka wa fedha 2024/2025 amesema serikali kupitia Tume imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa mabwawa saba na katika mabonde ya Lunguya, Mwamkanga, Amani, Ngaganulwa, Nimbo, Bulungwa na Kisuke.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live