Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SGR inavyoweza kuwa fursa kwa usafiri wa anga

Treni SGR SGR inavyoweza kuwa fursa kwa usafiri wa anga

Tue, 17 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya mtazamo kuwa, kuimarika kwa usafiri wa reli ya kisasa (SGR) kutaathiri usafiri wa anga kwa upande mmoja, wadau wa usafiri huo, wamesema reli hiyo ya kisasa inaweza kuimarisha sekta ya anga pia.

Matumaini ya wadau hao yanatokana na mtazamo, kuna uwezekano wa vyanzo hivyo vya usafiri kushirikiana na kuwapa fursa wananchi kuchagua aina gani wanayopenda kulingana na mahitaji yao.

Hoja hizo za wadau zinakuja katika kipindi ambacho, treni za SGR zimeteka soko la sekta ya usafiri kutokana na gharama nafuu, ufanisi na ratiba za kuaminika, jambo linalovutia abiria wengi.

Katika siku za karibuni, Shirika la Reli Tanzania (TRC) liliripoti kuhudumia abiria 366,000 tangu treni hiyo ilipoanza kutoa huduma kwa njia za Dar es Salaam- Morogoro na Dodoma.

Idadi hii imezidi matarajio ya awali na makadirio yanaonesha idadi ya abiria inaweza kufikia au kuzidi milioni moja katika miezi ijayo.

Uimara na ushawishi huo wa usafiri wa njia ya reli ya kisasa, haujawa tishio kwa wadau wa usafiri wa anga, wanaoonyesha matumaini ya kuimarika pia na kuwapa abiria fursa ya kuwa na machaguo ya aina ya usafiri.

Tishio la athari katika usafiri wa anga kama matokeo ya uimara wa SGR, linathibitishwa na mmoja wa abiria aliyeomba hifadhi ya jina lake, akisema ndege aliyopanda Jumamosi usiku kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, kulikuwa na abiria 10 pekee.

Hilo lilimpa wasiwasi kwa kile alichoeleza, kuna uwezekano safari hizo zikapotea, kwa kuwa, kwa kawaida ni hasara kwa ndege kupakia abiria chini ya 50.

“Ingawa SGR inaweza kutoa changamoto, hasa kwa abiria wa daraja la juu ambao kwa kawaida hushika nafasi zao mapema, haipaswi kuonekana kama mbadala wa moja kwa moja wa safari za anga,” amesema.

Ameongeza mashirika ya ndege yanayohudumia maeneo kama Dodoma yanapaswa kufikiria kuratibu ratiba zao na huduma za treni ili kudumisha faida.

Wasiwasi wake unaakisi suala pana zaidi, hasa mabadiliko yanayoweza kutokea ya abiria wa daraja la juu kutoka kwenye ndege kwenda kwenye treni.

Mabadiliko haya yanaweza kuwa changamoto kwa mashirika ya ndege, hasa katika njia maarufu kama ya Dodoma-Dar es Salaam, ambapo ndege huwa zimejaa lakini sasa zinakabiliwa na ushindani kutoka kwa huduma ya treni.

“Iwapo SGR itaendelea kuwa na ufanisi wa hali ya juu, huenda kukawa na kupungua kwa safari za ndege za Dodoma - Dar es Salaam kwani abiria wengi watapendelea kutumia treni.Tofauti kati ya kusafiri kwa treni na ndege ni ndogo na urahisi unaotolewa na treni za umeme unaweza kuathiri usafiri wa anga,” anasema.

Ingawa kwa abiria huyo ni wasiwasi, Mtaalamu wa Usafiri waAanga, John Njawa kwake ni matumaini, akipendekeza SGR inapaswa kuangaliwa kama nyongeza ya safari za anga badala ya kuwa mshindani wa moja kwa moja.

Hata hivyo, anasema kuanzishwa kwa SGR kunaweza kubadilisha mwamko wa abiria kwa muda, lakini haiwezekani kuathiri moja kwa moja usafiri wa anga, akisisitiza njia zote za usafiri zinaweza kuishi pamoja.

“Watu wana ladha tofauti na inahusu tabia ya wateja. Kitu kipya kinapotokea, watu wanataka kukijaribu,” amesema.

Njawa alikubali sekta ya usafiri wa anga hatimaye itaweza kuendana na kuwepo kwa SGR.

“Patakuwa na athari, hasa kwa muda mfupi, lakini hazitakuwa endelevu kwa muda mrefu. Ninaona huduma ya SGR kama nyongeza ya sekta ya usafiri wa anga badala ya mshindani wa moja kwa moja,” amesema.

Mtaalamu mwingine wa usafiri wa anga na mkufunzi, Juma Fimbo anaamini SGR ambayo bado iko katika hatua za mwanzo, haijawa changamoto kwa mashirika ya ndege.

Anaeleza huduma za reli hazina sera kamili za kushughulikia ucheleweshaji na usumbufu mwingine mdogo, maeneo ambayo mashirika ya ndege yameanzisha mikakati thabiti ya huduma kwa wateja.

“Kwa sasa hakuna ushindani halisi kati ya SGR na ndege; wako kama marafiki. Kuna uwezekano wa abiria kuchanganya safari za ndege na safari za SGR kwa usafiri wa ndani. Sekta zote mbili zinaweza kushirikiana kuboresha uzoefu wa usafiri,” amesema Fimbo.

Anaona uwezekano wa ushirikiano wa baadaye mashirika ya ndege na SGR yanaweza kuwa na huduma za pamoja za tiketi na kugawana mapato, hivyo kuzinufaisha sekta zote mbili.

Mtazamo huo, unaungwa mkono na rubani wa ndege, Philemon Kisamo anayesema abiria wengi kwa sasa wanapendelea SGR kwa sababu ya bei nafuu ukilinganisha na tiketi za ndege.

Mara kwa mara za safari za SGR kila siku zinatoa urahisi kwa wasafiri wa muda mfupi, kama wale wanaosafiri kibiashara.

“Ingawa mabasi yaendayo mikoani yanaweza kutoa nauli za chini zaidi, SGR ni ya kasi zaidi na abiria wanathamini uratibu wake wa muda. Ningeshauri SGR kudumisha kiwango hiki cha huduma,” amesema.

Wadau wa usafirishaji

Meneja wa masoko na mawasiliano ya ushirika wa Precision Air Tanzania, Hilary Mremi anasema badala ya kuiona SGR kama tishio vema itazamwe kuwa fursa.

Anasema itazamwe kama fursa itakayofanya mashirika ya ndege kuboresha huduma zao: “Kwa kuboresha ubora wa usafiri wa anga, mashirika ya ndege yanaweza kuendelea kutoa sababu zinazovutia kwa abiria kuchagua ndege badala ya treni.”

“Tunaona SGR kama changamoto chanya ambayo itatusukuma kuboresha huduma zetu, na kuzifanya kuvutia zaidi kwa abiria, hasa ukizingatia muda mfupi wa safari za ndege ukilinganisha na treni,” amesema Mremi.

Ameongeza athari za SGR ni ndogo kwa sasa na idadi ya abiria bado inabadilika akitoa mfano:“Safari za ndege kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam huwa zimejaa siku za Ijumaa na kupungua kwa abiria siku za Jumamosi si jambo geni.”

Kama sehemu ya kukabiliana na athari za SGR, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimetangaza mipango ya kuendeleza mikakati ili kuendelea kushindana, ikihusisha kuhamisha mitaji yao katika maeneo mengine ya uwekezaji.

Katibu Mkuu wa Taboa, Joseph Prisicus amebainisha chama hicho kinaangalia namna ya kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwamo kuomba msamaha wa kikodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na kupungua kwa shughuli za mabasi.

“Hatuwezi kupinga maendeleo ya reli. Kuna faida nyingi kama abiria wataishia Dodoma na kuna mabasi ambayo yatawachukua kwenda maeneo mengine. Kwa kuwa sisi sote ni walipakodi, Serikali inapaswa kuangalia jinsi ya kuwasaidia wamiliki ili wote wanufaike,” anasema Prisicus.

Prisicus anasema Taboa inachunguza athari kwenye ajira na mitaji ya wawekezaji na inaweza kurekebisha shughuli zao kulingana na matokeo ya uchunguzi.

Kuanzishwa kwa SGR kumesababisha baadhi ya wamiliki wa mabasi kupunguza safari zao.

Kwa mfano, kampuni iliyokuwa ikifanya safari 20 kwa siku kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro sasa imepunguza hadi safari tisa au 10 kwa siku. Kupungua huku kwa huduma kuna athari kwa malipo ya kodi na uendelevu wa uendeshaji.

Kadiri SGR inavyoendelea kuimarika na kupanuka, uhusiano wake na sekta ya usafiri wa anga unaweza kubadilika.

Ingawa kuna wasiwasi kuhusu ushindani, wataalamu wanakubaliana kwamba kuna fursa ndani yake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live