Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruksa korosho kusafirishwa bandarini Dar

Video Archive
Sun, 31 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Serikali imeruhusu korosho inayonunuliwa na wafanyabiashara katika msimu huu wa 2021/22 kusafirishwa katika bandari ya Dar es Salaam na Mtwara.

Naibu waziri wa kilimo Hussein Bashe ametangaza uamuzi huo wa serikali mapema leo Jumapili Oktoba 31, 2021.

"Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uamuzi huo baada ya kusikiliza maoni ya wafanyabiashara kufuatia changamoto kubwa ya upatikanaji wa makasha na meli unaoikumba dunia kwa sasa na kupanda kwa gharama za usafirishaji kwa njia ya bahari," amesema Bashe.

Bashe amesema gharama za kusafirisha tani moja ya korosho kwa kutumia bandari ya Mtwara sasa hivi ni dola za Marekani 120 hadi 180 kutegemeana na aina ya meli mfanyabiashara anayotumiwa ya makasha (container vessel) au ya kichele (bulk cargo vessel) ambayo ni ongezeko la zaidi ya dola za kimarekani 100 katika bandari ya Dar es Salaam.

Pia gharama za usafirishaji katika bandari ya Mtwara kwa tani moja ni dola ya Marekani 120 hadi 180 huku katika bandari ya Dar es Salaam ni dola za kimarekani 74.

Bashe amesema ili pia kumfanya mfanyabiashara asibebe gharama kubwa ambayo itaathiri bei ya mkulima wa korosho sokoni imeamua kuruhusu matumizi ya bandari zote mbili za Mtwara na Dar es Salaam.

Amesema ni matarajio ya Serikali kwamba wanunuzi wa korosho watatoa bei shindani katika minada ya korosho inayoendelea katika mikoa ya kanda ya kusini na kuahidi kuwa Serikali haitaingilia utaratibu wa soko.

Chanzo: mwananchidigital