Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mghwira afagilia uwezo wa TSN ataka ijitangaze

B32765428b9ec83bcb3285c7e59e175e RC Mghwira afagilia uwezo wa TSN ataka ijitangaze

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira amepongeza ubunifu na umakini wa utendaji kazi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali(TSN) katika upashaji wake wa habari na kuitaka kujitangaza zaidi ili ipatiwe kazi nyingi za uchapishaji wa majarida na bidhaa nyingine.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa mwito huo jana wakati akizungumza na viongozi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali(TSN) wachapishaji wa magazeti ya Dailynews, HabariLeo, HabariLeo Afrika Mashariki ,Sundaynews, HabariLeo Jumapili na SportsLeo katika makao makuu ya kampuni hiyo yaliyopo Tazara, Temeke- Dar es Salaam.

Alisema licha ya uwapo wa vyombo vingi vya habari nchini, bado magazeti hayo yanaaminiwa kwa kuwa na habari za ubora na zinazoaminiwa zaidi na wasomaji huku akipongeza ubunifu wake uandishi katika magazeti hayo na huduma zake za mtandaoni.

Mghwira ambaye alipata wasaha wa kutembelea mtambo wa kuchapisha magazeti, aliishauri kampuni hiyo kujitangaza zaidi huduma zake zinufaishe watanzania wengi zikiwamo taasisi na mashirika ya serikali.

Akizungumzia mchango wa mkoa katika kukuza uchumi wa nchi, alisema wanawekeza zaidi katika sekta ya madini yanayopatikana wilayani Same pamoja na tangawizi na vanila.

Alisema kwa miaka miwili tangu kugundulika kwa madini hayo, mkoa umefungua vituo vya kuuzia. Alisema katika kuhakikisha inawawezesha wananchi kukua zaidi kiuchumi, mkoa umewawezesha kupata vibali vya kwenda kuuza madini mikoa ya jirani ambapo wengi wao wameonekana kunufaika zaidi.

Kuhusu tangawizi, alisema inachangia ajira kwa wakazi wa Same kwa kuwa wapo wanaouza hadi nje ya wilaya. Alisema zao vanila linazidi kushika kasi na kuvutia zaidi wakulima waliokuwa wakilima kahawa kukimbilia kwenye kulima zao hilo, wameona faida ya uuzwaji wa zao .

Alisema mkoa una mashamba makubwa yanayoajiri watu zaidi ya 2,000 huku akitolea mfano wa shamba la maua lililoajiri watu 800.

Alionesha kukerwa na kukosekana kwa viwanda vya kutosha katika mkoa huo. Mghwira alisema mkoa umeamua kukuza zaidi sekta ya mifugo hasa mifugo ya kienyeji kuchagiza ajira kutokana na viwanda vitakavyojengwa

. Aliwahakikishia uhakika wa umeme wa kutosha. Katika msafara wake huo aliongozana na Meneja Mkuu wa Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro, Godfrey Ng’urah ambaye alibainisha kuwa benki hiyo imenuia kuinua uchumi wa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa mingine kupitia vyama vya ushirika huku akiwahakikishia wananchi huduma bora.

Chanzo: habarileo.co.tz