Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB yaunga mkono agizo la Majaliwa

716c4d87e8cd1d5f70c370a9f2d0a6cf NMB yaunga mkono agizo la Majaliwa

Sun, 17 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BENKI ya NMB imetoa msaada wa mabati 400 kwa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, ikiunga mkono utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilolitoa kwa mikoa yote nchini yenye upungufu wa vyumba vya madarasa kuhakikisha ifikapo Februari 28, mwaka huu, vimejengwa na wanafunzi wako masomoni.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo Desemba 7, mwaka jana wakati akizungumza na wakuu wa mikoa, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), ili kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza waliofaulu wanakuwa masomoni wote.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu Majaliwa Waziri Mkuu aliagiza Ofisi ya Rais (Tamisemi), ihakikishe kazi hiyo inakamilika kwa wakati na aliwataka watendaji hao wahakikishe ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na utengenezaji wa madawati vinafanyika usiku na mchana.

Ili kuhakikisha agizo hilo la Waziri Mkuu linatakelezwa kwa haraka, benki hiyo ya NMB imetoa msaada huo jana wilayani Urambo ambao thamani ya mabati hayo ni Sh milioni 15.

Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa wilaya hiyo, Angelina Kwingwa, Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi, Sospeter Magese alisema mbali na kurejesha faida kwa jamii, benki hiyo imeona kuna haja ya kuunga mkono utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu.

Magese alisema baada ya kusikia wito wa Waziri Mkuu Majaliwa akisisitiza wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza lazima waanze masomo hawakusita kutoa msaada kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.

“Kupitia msaada huu ambao Benki ya NMB imetoa kwenu, ni matumaini yetu kuwa wilaya hii inaenda kutekeleza agizo la kiongozi mkuu, kwa wakati na kwa haraka kama ambavyo aliagiza na wanafunzi waweze kuanza masomo,” alisema Magese.

Akipokea msaada huo, DC Kwingwa ameishukuru benki hiyo kwa kuendelea kuwasaidia wananchi na kueleza kuwa NMB imemwondolea aibu kwa kumvika nguo, na kuwa msaada huo umefika wakati mwafaka na kuwataka wadau wengine kuiga mfano wa benki hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya amewaonya wanafunzi kutotumia meza na viti ili vidumu kwa muda mrefu kutokana na tabia ya baadhi yao kupanda juu yake na kusababisha kuharibika.

Wakati huo huo, benki hiyo imetoa msaada wa dharura wa vifaa mbalimbali kwa wakazi wa Kijiji cha Kipera na Kitongoji cha Kinyenze, Kata ya Mlali Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro baada ya kaya 54 kuathirika na mvua iliyoambatana na upepo mkali kuezua mapaa na kubomoa nyumba Januari 9, mwaka huu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa mkuu wa wilaya hiyo katika Kijiji cha Kipera mkoani hapa, Meneja wa benki hiyo Kanda ya Mashariki, Dismas Prosper alisema baada ya kupata taarifa ya wakazi hao kupata janga hilo, benki hiyo imetoa msaada wa dharura wenye thamani ya Sh milioni tano.

Dismas alisema vifaa hivyo ni magodoro 54, mashuka 110, mchele kilo 540, lita 110 ya mafuta ya kula na sukari 160 kwa ajili ya kugawiwa kwa walengwa katika kipindi hiki kigumu.

“NMB imekuwa ikitoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa jamii hasa wanapopata janga mbalimbali na leo tumetoa vifaa muhimu vyenye thamani ya shilingi milioni tano ambao tunaamini uongozi utawagawia walengwa katika kipindi hiki kigumu,” alisema Prosper.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mlali, Anuciata Mpina alisema Januari 9, mwaka huu, mvua kubwa iliyoambatana na upepo ilinyesha na kusababisha madhara kwa kaya 54 ambazo nyumba zimebomoka na kuezuliwa mapaa huku watu 318 wakikosa makazi.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Albanus Mgonya alisema baada ya kutokea kwa janga hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ilitembelea nyumba za waathirika 318 na kuwataka watu wote ambao wamekumbwa na janga hilo wasirejee katika nyumba ambazo zimebomoka upande mmoja.

Mgonya aliishukuru NMB kwa msaada huo ambao unaenda kuwaokoa wananchi ambao walikubwa na janga hilo, ambalo alieleza limewaacha bila ya chakula ambacho walikuwa wameweka akiba.

Chanzo: habarileo.co.tz