Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwigulu aibuka utata wa sh trilioni 1.7

Makipo Ya Watoa Huduma Huzingatia Masharti Ya Mikataba   Mwigulu Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

Mon, 22 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Saa chache baada ya kuripotiwa kuhusu likichokiita utata wa Sh. trilioni 1.7 kutolewa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba ameibuka na kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.

Katika toleo lake la jana, gazeti hilo liliripoti kuwa Sh. trilioni 1.7 zilizotolewa BoT katika mwaka 2022/23 na kutumiwa na serikali ilhali hazikuwa sehemu ya makusanyo ya serikali kwa mwaka huo wa fedha.

Katika ufafanuzi wake kupitia mitandaoni ya kijamii jana, Waziri Mwigulu alisema serikali ilichukua fedha hizo BoT kama "advances or short term loans".

Alitaka wananchi wapuuze suala hilo ambalo jana liliteka mijadala ya mitandao ya kijamii, akisisitiza BoT inasimamia kwa umakini sheria za nchi na miiko ya benki kuu zote duniani.

"Nimesoma taarifa hiyo (ya Nipashe Jumapili) ambayo inatokana na uchambuzi wa NGO iitwayo WAJIBU inayoongozwa na Mzee Ludovic Utuoh, CAG mstaafu.

"Kwa ujumla, maelezo ya taarifa hiyo yanaeleweka na hayana utata wowote, hivyo sijui kwanini mwandishi wa Nipashe ameeleza kuwa kuna utata BoT. 

"Taarifa imeelezea suala ambalo ni la kawaida na huwa linafanyika kila mwaka kutokana na Sheria ya BoT inayoruhusu kutoa advances or short term loans kwa serikali ili kukidhi mahitaji ya matumizi ambayo yanakuwa hayajapata mapato. 

"Kwa mujibu wa kifungu cha 34 hadi 37 cha Sheria ya BoT, serikali inaruhusiwa kukopa hadi asilimia 18 ya makusanyo halisi ya ndani ya mwaka uliopita. 

"Hili limekuwa linafanyika hivyo tangu BoT ianzishwe. BoT ni benki ya serikali, serikali huchukua 'advance' kwa mujibu wa sheria badala ya kukopa riba kubwa kutoka benki za biashara. 

"Hivyo, kwa mwaka 2022/23, serikali ilikuwa inaweza kukopa BoT kiasi kinachofikia Sh. trilioni 4.5. Hivyo, taarifa ya kuwapo mkopo wa Sh. trilioni 1.7 ni suala ambalo liko ndani ya wigo unaokubalika kisheria.

"Kiasi hicho kilipofika mwisho wa mwaka kilijumuishwa kwenye 'Treasury Bonds' za mwaka husika ambazo zinaendelea kulipia riba kama sehemu ya mikopo ya ndani," alisema Dk. Mwigulu.

Aliendelea kueleza kuwa utaratibu huo ni wa kawaida na ufanyika kwa Benki Kuu za nchi nyingi duniani, pindi serikali inapohitaji fedha za kugharamia bajeti wakati bado inaendelea kujipanga na kukusanya mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali. 

"Ndio maana hata IMF waliridhika kuwa BoT na serikali wamezingatia sheria na taratibu za kimataifa kama inavyotakiwa. Kutokana na uzingatiwaji sheria hizo, Bodi ya IMF waliridhia kutoa USD milioni 300 kwa mwaka 2023/24 na Benki ya Dunia waliridhia kutoa USD milioni 750 kwa mwaka 2023/24," alisema.

Waziri Mwigulu alisema taasisi hizo ziliridhia kutoa fedha hizo kwa kuzingatia Tathmini ya Pili ya Programu ya IMF iliyofanyika Desemba 2023 iliangalia masuala mbalimbali yakiwamo ya mapato, matumizi, madeni, uzingatiwaji Sheria ya BoT, ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, urari wa biashara, thamani ya Shilingi na usimamizi wa masoko ya fedha nchini. 

Dk. Mwigulu aliahidi BoT itaandaa taarifa kwa umma na kutoa elimu, akisisitiza ni serikali kuchukua 'advance' ya Sh. trilioni 1.7 Benki Kuu "ni suala la kawaida".

Katika ripoti yake jana, gazeti Nipashe Jumapili liliripoti kuwa uchambuzi wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23 uliofanywa na Taasisi ya WAJIBU umebaini kuwa mwaka huo wa fedha, serikali iliidhinishiwa na Bunge kukusanya na kutumia Sh. trilioni 41.48.

Hata hivyo, ukaguzi wa CAG kuhusu Hesabu za Serikali Kuu kwa mwaka 2022/23, ulibaini serikali ilikusanya Sh. trilioni 41.88, kukiwa na ziada ya Sh. bilioni 400.

Vilevile, makusanyo yaliyopelekwa Mfuko Mkuu ni Sh. trilioni 38.447. Sh. trilioni 3.433 hazikupita Mfuko Mkuu wa Serikali.

Uchambuzi ukabaini kuwa serikali licha ya kukusanya trilioni 38.447 zilizopita Mfuko Mkuu, BoT iliipa (serikali) Sh. trilioni 40.18, hivyo Benki Kuu kuipa serikali Sh. trilioni 1.7 za ziada, zilizozua utata, hadi jana Waziri Mwigulu alipofafanua kuwa "serikali ilikopeshwa fedha hizo na BoT".

Vilevile, uchambuzi umebaini kuwa kati ya Sh. trilioni 3.433 ambazo hazikupita Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mwaka huo wa fedha, Sh. trilioni 3.197 zilipelekwa moja kwa moja kwenye miradi.

RIPOTI YA CAG Inaporejewa Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2022/23 kuhusu suala hilo, inaonesha kuwa katika mwaka huo wa fedha, serikali ilikusanya Sh. trilioni 41.880 ikiwa ni zaidi ya bajeti ya Sh. trilioni 41.480 kwa Sh. bilioni 400.

CAG anafafanua kuwa kati ya Sh. trilioni 41.880 zilizokusanywa, Sh. trilioni 38.447 zilipokewa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, hivyo kuwapo tofauti ya Sh. trilioni 3.4334.

CAG anasema tofauti hiyo inatokana na Sh. trilioni 3.656 zilizopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutoka kwa wadau wa maendeleo na makusanyo yaliyopelekwa Zanzibar ambayo hayapitii Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali pamoja na Sh. bilioni 223 zinazotokana na bakaa za makusanyo ya kodi za mwaka uliopita na makusanyo mengine yaliyopokewa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali nje ya makisio ya bajeti.

"Jumla ya matumizi yaliyofanywa katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ili kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/23 yalikuwa Sh. trilioni 39.523 bila kujumuisha Sh. bilioni 665.80 zilizotolewa kama fedha zilizorejeshwa (refunds) na matumizi mengine kwenye jumla ya makusanyo ya Sh. trilioni 38.447, hivyo kusababisha nakisi katika Benki Kuu (BoT) ya Sh. trilioni 1.742 kufikia tarehe 30 Juni 2023," CAG anaeleza katika Ripoti yake ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live