Dar es Salaam. Nini kipo nyuma ya zao la korosho? Ndiyo swali kubwa katika sakata la korosho lililoanza tangu wakati wa Bunge la Bajeti hadi Rais John Magufuli alipoamua kuingilia kati Ikulu juzi.
Katika kipindi hicho cha Bunge la Bajeti mwaka huu, wabunge kutoka mikoa inayozalisha kwa wingi zao hilo walijaribu bila mafanikio kuzuia mabadiliko ya sheria yaliyoondoa mgawo wa ushuru wa kuuza nje kwenda mfuko wa zao hilo.
Bunge likapiga kura ya kupitisha mabadiliko hayo, huku wabunge wa CCM wakitakiwa kuhudhuria bila ya kukosa na wale waliokosa walitakiwa wajieleze.
Na baada ya Bunge, mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia na makamu wake, Jitu Soni, ambao walikuwa mstari wa mbele katika sakata hilo walijiuzulu nyadhifa zao.
Pia minada mitatu ya korosha ya Tandahimba na Newala; Masasi na Mtwara; na Ruangwa, Nachingwe na Liwale, ilikwama baada ya wakulima, ambao mwaka jana walijivunia mamilioni ya fedha kutokana na bei safi iliyofikia zaidi ya Sh3,000 kwa kilo, kukataa bei mpya ya chini ambayo ni kati ya Sh1,700 na Sh2,700 kwa kilo.
Na juzi mchana, kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alichambua kukwama huko kwa minada ya korosho akihusisha na makosa ya Serikali kutosikiliza wabunge.
Katika kikao cha Serikali na wanunuzi wa zao hilo juzi, Rais Magufuli aliagiza bei ya korosho itakayonunuliwa kwa wakulima isipungue Sh3,000 na kwamba iwapo wafanyabiashara hao watang’ang’ania bei, Serikali inaweza kununua na kutafuta soko zuri yenyewe.
Mazao mengine ya biashara huporomoka bei na maisha huendelea, lakini kwa korosho hali imekuwa tofauti.
Wachambuzi waliozungumza na Mwananchi jana walisema korosho imetikisa kila kona nchini kwa kuwa ni zao linaloingizia Taifa mapato makubwa na hivyo Serikali ilipaswa kusikiliza kilichoshauriwa na wabunge.
“Korosho ndio zao ambalo linauzika kwa kiasi kikubwa nchini ukilinganisha na mazao mengine,” alisema Dk Donath Olomi, ambaye ni mchumi na mtaalamu wa biashara.
Alisema mpaka sasa wajanja wengi wanalitegemea zao hilo ili kujiinua kiuchumi, lakini ni vyema kukawa na mfumo wa sheria usiobadilika, sheria ambazo zitawavutia wawekezaji wa zao la korosho ili kuinua uchumi wa nchi na hata nchi kupata mapato.
Maoni kama hayo alitoa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda aliyesema kwa kuwa korosha inaingiza fedha nyingi, Serikali inatakiwa kusikiliza hoja za wabunge na wakulima wa zao hilo.
Alisema hali inaonyesha kuwa wabunge walipuuzwa na ndio maana zao hilo linaonekana halina maana. “Hii ndio ilisababisha hata mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge akajiuzulu. Hivyo ni fundisho kwa Serikali kujua kama hilo zao lina manufaa kwa wananchi,’’ alisema.
Naye Mkurugenzi wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte alisema hoja za wabunge zilitakiwa kusikilizwa katika kutatua matatizo ya zao hilo hapa nchini ili kuwanufaisha wakulima na kukuza uchumi wa nchi.
Wakati wa Bunge la Bajeti, wabunge walipinga mabadiliko ya sheria ambayo yalifuta mgawo wa asilimia 65 za ushuru wa korosho inayouzwa nje kwenda Mfuko wa Maendeleo ya Korosho na asilimia zilizobaki kwenda Serikalini.
Walisema mgawo huo ulisaidia wakulima kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na pembejeo na kwamba ulianzishwa kwa mapendekezo ya wadau wa korosho, tofauti na mazao mengine yanayouzwa nje.
Kuhusu kitendo cha Rais kuruhusu wafanyabiashara kuwekeza katika viwanda vya kubangua korosho, mkurugenzi huyo wa TPSF alisema kitanufaisha wakulima na kuongeza Pato la Taifa.
Alisema wakulima wa zao hilo walishasahaulika kwa kiasi kikubwa ndio maana hata suala la bei liliwakosesha amani.
“Rais kaingilia kati suala hili limekuwa faraja kwa wakulima na pia watajituma sasa baada ya kuanza kukumbukwa,’’ alisema Shamte.
Alisema mazao yao mengi yalikuwa yanaozea shambani kutokana na kupangiwa bei.
Mmoja wa wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi alisema kuna uwezekano mdogo kwa bei hiyo kupanda.
“Bei haiwezi kuvuka Sh3,000 kwa sababu bei ya ndani inategemea soko la dunia. Kwa sasa soko la dunia ni kama dola 1.6 za Kimarekani (sawa na Sh3,600 hadi Sh4,000 kwa kilo),” alisema mfanyabiashara huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
“Makato ya export levy yametoka Sh600 hadi Sh1300 kwa kilo moja, ambayo anailipa msafirishaji ambaye sasa ndiye mnunuzi. Kwa hiyo ili naye apate faida, lazima amkandamize mkulima.
“Kinachopaswa kufanywa na Serikali ni kupunguza kodi zake. Kwa hali ilivyo sasa mkulima ataendelea kuumia na huo mnada unaokuja hautaweza kufanyika au kuongeza bei hadi kufikia Sh4,000 au Sh5,000 kwani itakuwa hasara mnunuzi.”
Hata hivyo, juzi Rais alitangaza kupunguza baadhi ya tozo zinazoumiza wanunuzi, ikiwa ni pamoja na ushuru wa halmashauri ambao ulikuwa ukitozwa na halmashauri tofauti kwa shehena moja.
Naye mkurugenzi wa Sera wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Akida Mnyenyelwa alisema huwezi kulinganisha korosho na mazao mengine yanayolimwa nchini kwa kuwa linaingiza fedha nyingi.
Alisema wamepokea kwa mikono miwili ujumbe wa Rais na wanaufanyia kazi kwa haraka kwa kuanza kutafuta wawekezaji nchini wa zao hilo.
“Hiki ni kilio chetu cha muda mrefu hivyo kwa agizo hili la kiongozi wetu wa nchi tutahakikisha tunapata wawekezaji wa zao hili, na si korosho tu bali hata mazao mengine,’’ alisema.
Lakini, Zitto alikuwa na maoni tofauti juzi mchana ikiwa ni muda mfupi kabla ya Rais kutoa maagizo yake kwa wafanyabiashara.
Katika mkutano na waandishi wa habari, mbunge huyo wa Kigoma Mjini na ambaye alikuwa miongoni mwa wabunge walioibana zaidi Serikali bungeni kuhusu korosho, alisema Serikali haipaswi kukwepa lawama kwenye suala la uuzaji wa korosho na ni vizuri ikubali kuwa imefanya makosa.
“Badala ya Serikali kulichukulia zao la korosho kama la kimkakati imekuwa haisikii, haielewi na sasa imeharibu kuku anayetaga mayai ya dhahabu katika nchi yetu,” alisema.
Alisema korosho ndio zao pekee la kuiokoa nchi na kupingana na habari kwamba Serikali imepata wanunuzi wa korosho kutoka Marekani watakaonunua kilo moja kwa Sh5,000.
Zitto alisema taarifa alizonazo kutoka Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na wanunuzi, uzalishaji wa zao hilo utashuka kwa asilimia 40.
“Mnaweza kuona fedha za kigeni tunazoenda kupoteza kwa uamuzi wa Serikali kuchukua fedha zote za export levy (ushuru wa mauzo nje) badala ya kupeleka zinakostahili,” alisema.
Mjadala wa zao hilo, ambalo sasa linalimwa mikoa mbalimbali nchini lakini kitovu kikiwa ni Lindi na Mtwara ulianza kushika kasi bungeni.
Hoja za wabunge hao zilizofikia hatua ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuonywa aifanye ziara mikoa ya kusini, hazikuweza kufua dafu na sasa Serikali inachukua asilimia 100 ya fedha za ushuru wa zao hilo.
Baada ya Bunge, Rais John Magufuli alisema katika moja ya mikutano ya hadhara kuwa alipanga kuwatimua uanachama wa CCM wabunge wa mikoa ya Lindi na Mtwara akiwamo Waziri Mkuu, Majaliwa kama sheria hiyo isingepita.
Siku kadhaa baadaye, Ghasia na Soni walitangaza kujiuzulu nafasi zao kwenye Kamati ya Bajeti ya Bunge, bila kuhusisha uamuzi wao na sakata la korosho.
Wakati hali ikionekana kuanza kutulia, wakulima mkoani Mtwara waligomea mnada wa korosho na kufuatiwa na mgomo kama huo katika minada mingine miwili, kabla ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kufanya kikao na wakuu wa mkoa inayolima korosho kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Katika kikao hicho, aliagiza wizara ya kilimo kumrudisha wizarani aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Profesa Wakuru Magigi baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Wakati Majaliwa akitoa maagizo hayo, juzi Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na wadau wa korosho na kutoa msimamo wa Serikali kuhusu bei kuwa ni lazima isiwe chini ya Sh3,000.
“Kama hamtanunua korosho kwa bei yenye maslahi kwa wakulima, Serikali itanunua korosho kwa bei nzuri kwa wakulima na tutaihifadhi,” alisema Rais.
“Nipo tayari hata kutumia majeshi yetu kununua korosho na tutatafuta masoko ya uhakika ili tuuze kwa bei nzuri.”