Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkutano Mkuu wa Wahasibu Afrika kufanyika Arusha

Uchumi Kupanda Mkutano Mkuu wa Wahasibu Afrika kufanyika Arusha

Thu, 25 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu Barani Afrika (African Association of Accountants General Meeting (AAAG)) utakaofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 3 hadi 5 Disemba mwaka 2024, ukiwahusisha zaidi ya washiriki 2,000 kutoka takribani nchi 55 za Bara la Afrika.

Hayo yameelezwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Arusha, uliolenga kuujulisha umma kuhusu mkutano huo na fursa za kiuchumi na kijamii kwa Watanzania.

CPA Mkude alisema kuwa mkutano huo unatarajia kuleta manufaa makubwa kiuchumi na kijamii pamoja na kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania, hususanI kwa wajumbe kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko katika ukanda wa Kaskazini.

Alizitaja faida nyingine za mkutano huo kuwa ni pamoja na kuwa na Afrika yenye mafanikio yenye msingi wa ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu, Bara jumuishi lililounganishwa kisiasa na kwa kuzingatia maadili ya Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism).

Ameyataja manufaa mengine kuwa ni pamoja na kuwa na maono ya mwamko wa Afrika na Afrika yenye utawala bora, demokrasia, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria, Afrika yenye amani na usalama na Afrika yenye utambulisho thabiti wa kitamaduni, urithi wa pamoja na maadili.

CPA Mkude amesema kuwa mkutano huo utawaleta Wahasibu Wakuu wa Serikali Afrika watakaoambatana na Wahasibu Wakuu wa Wizara, taasisi za umma na wahasibu na wadau wengine ambao watapata fursa ya kusikiliza mada za masuala mbalimbali ya kitaaluma na kubadilishana mawazo na kujua fursa zinazopatikana katika nchi za Afrika.

Alisema wageni kutoka nje watakuja na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa Tanzania kwa kuwa watatembezwa kwenye mbuga za wanyama na vituo mbalimbali vya utalii na hivyo kuunga mkono dhamira ya Rais ya kuutangaza Utalii wa Tanzania.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa nyumba za wageni (hoteli), usafiri, mama lishe na jamii kwa ujumla kuchangamkia fursa hiyo ya ujio wa wageni ili kunufaika kiuchumi na kijamii.

“Ninatoa wito kwa Maafisa Masuuli wa Wizara na Taasisi zote kuwaruhusu wahasibu, wakaguzi na wadau wengine watakaoomba kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali Afrika, African Association of Accountants General (AAAG) utakaofanyika jijini Arusha mwezi Disemba, 2024”, Amesema CPA Mkude.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wahasibu wa Afrika ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa nchi ya Lesotho, Bi. Malehlohonolo Mahase amesema Mkutano wa Wahasibu Afrika unafanyika Tanzania kwa kuwa ni mwanachama anayeaminika na amekuwa mshiriki mwaminifu katika umoja huo, na kwamba wajumbe wa mkutano huo wanakuja kujifunza namna Tanzania ilivyopiga hatua kubwa katika matumizi ya mifumo ya fedha.

Alisema kuwa Tanzania ipo vizuri katika kutekeleza viwango vya kimataifa vya kihasibu, imekuwa ya mfano katika ukuaji wa Uchumi, imeimarika katika suala la ukarimu wa wageni, maendeleo katika teknolojia ya Habari na Mawasiliano na ni miongoni mwa nchi zenye vivutio vingi vya utalii hivyo wanachama kuna mambo mengi ya kujifunza.

Aidha alieleza kuwa Mkutano huo utakao wakutanisha pia Jumuiya za wafanyabiashara watapata fursa ya kujua ni namna gani Afrika ipo tayari katika suala la uwekezaji na namna ya kuripoti hali ya uchumi ya Afrika, jambo ambalo litaongeza uwazi na uwajibikaji.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Bi. Christine Mwakatobe amesema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wageni wanapokuja wanapata huduma bora kwa kuwa wanaamini watakuwa mabalozi wa Tanzania na watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

Amesema anamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuitangaza nchi ya Tanzania duniani na kwamba hayo ni matunda ambayo Taasisi za Serikali kwa ujumla zinafaidi kwa kazi yake anayoifanya, huku kituo chake cha mikutano kikihudumia mikutano mingi ya Kitaifa na Kimataifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live