Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mavunde awaonya wamiliki leseni uchimbaji madini

Mavunde Na Madini Waziri wa Madini, Antony Mavunde.

Wed, 26 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Madini, Antony Mavunde, amewaonya wamiliki wa leseni za uchimbaji madini nchini kuacha kuichonganisha serikali kwa kuingia mikataba kinyemela na wachimbaji wadogo na wawekezaji wenye mitaji mikubwa.

Mavunde alitoa onyo hilo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa mgodi wa Ntambalale namba mbili uliopo Kijiji cha Wisolele Kata ya Segese, Halmashauri ya Msalala wilayani hapa Mkoa wa Shinyanga kuhusu mikakati ya serikali kuhakikisha kila mmoja ananufaika na rasilimali hiyo.

Alifafanua kuwa ametoa onyo hilo baada ya serikali kubaini kuwa baadhi ya wamiliki hao wa leseni wamekuwa chanzo kikubwa cha kuichonganisha na wachimbaji wadogo kwa kuwaingiza kwenye maeneo yao na kuanzisha uchimbaji kwa kupeana mirabaha.

Alisema wamiliki hao baada ya kupata wawekezaji wenye mitaji mikubwa, wanakimbilia kwa wakuu wa wilaya kuomba msaada wa askari wa Jeshi la Polisi kuwaondoa wachimbaji hao wadogo kwa nguvu.

Waziri huyo alisisitiza kuwa watakaobainika kuwaweka wachimbaji kwenye maeneo yao kinyemela, serikali itawanyang’anya leseni na kuwapatia wachimbaji waliojiunga kwenye vikundi.

Alisema sheria inamtaka mmiliki kuchimba madini mwenyewe na sio kuingia ubia kinyemela na wachimbaji, kisha kuwaondoa kwa nguvu wanapopata wawekezaji hao, wenye mitaji mikubwa.

“Yeyote mwenye leseni asiingize wachimbaji kwenye leseni yake na kuanza kuchimba madini, jukumu la kulinda leseni isivamiwe ni la mwenye leseni mwenyewe, kama utaingia ubia na wachimbaji hakikisha unafunga mkataba wa kisheria kuondoa migogoro hapo baadaye," alisema Mavunde.

Kwa mujibu wa Mavunde, bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha wa 2024/25 imeongezeka kutoka Sh. bilioni 89 mpaka Sh. bilioni 231 kwa ajili ya kuziwezesha taasisi ya utafiti wa madini na miamba, kununua helikopta ya kufanya utafiti wa maeneo yenye madini na kuwapatia wachimbaji ili kuondoa dhana ya kubahatisha.

Mchimbaji wa mgodi huo, Adrian Lugola, alisema wamekuwa wakiibua maeneo yenye madini na wanapoungana na kikundi kuomba leseni wanaambiwa ni eneo la mtu.

Aliiomba serikali kuyafuta maeneo ambayo hayajaendelezwa na kupewa wachimbaji ili wajikwamua kiuchumi.

Bangili Mkongwe, alisema ili kuondoa matumizi ya kemikali ya Zebaki, ambayo yamekuwa yakihatarisha usalama wa maisha yao kwa kukamata madini bila kuchukua tahadhari, serikali ifunge mashine ya kusaga mawe yenye dhahabu na uchenjuaji wilayani Kahama.

Alisema mashine kama hizo ambazo zimefungwa Katoro mkoani Geita na Itumbi Wilaya ya Chunya Mbeya zimepunguza majanga ya kemikali.

Alisema hivi karibuni Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) waliwatembelea na kuwapatia elimu dhidi ya athari ya zebaki.

Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Kahama, Joseph Kumburu, alisema mashine hiyo itafungwa na Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) hivi karibuni. Kumburu, alisema wako katika hatua ya usanifu na kwamba eneo la kuweka mashine hiyo imepatikana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live