Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano mkubwa wa kikanda unaohusisha wadau wa kilimo cha mboga mboga na matunda (Horticulture) katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika kesho katika Hoteli ya Regency jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Horticulture Association (TAHA), Dk Jaquiline Mkindi amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kufungua fursa za masoko na uwekezaji kwa wadau wa kilimo hicho katika kanda hizo.
“Nianze kwa kusisitiza kuwa dhima kuu ya mkutano huu ni kuhamasisha wawekezaji kwenye sekta ya ‘hortculture’ kwa wadau kutoka kanda hizi mbili pamoja na kuhamasisha watanzania kuwekeza katika kilimo hiki ambao wengi wao bado hawajatambua fursa mbalimbali zilizopo ndani yake” amesema Dk Mkindi.
Amesema washiriki watapata fursa ya kuelewa ni namna gani ya kutafuta masoko kutoka kwa wakulima, wasindikaji na wasafirishaji wakubwa wa mazao hayo kutoka kanda hizi mbili.