Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemtaka mkandarasi anayejenga machinjio ya kisasa ya Vingunguti jijini Dar es Salaam ahakikishe anakamilisha ujenzi huo mwishoni mwa Desemba 30, 2019 kama alivyoamriwa na Rais wa nchi hiyo, John Pombe Magufuli.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo leo Jumanne, Desemba 3, 2019, Majaliwa amesema amefurahishwa na hatua ya mkandarasi huyo ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ya kuongeza idadi ya watalaam na mafundi ili kuhakikisha kazi hiyo inafanyika haraka na kukamilika kwa wakati.
Amesema amefurahi pia kuona mkandarasi huyo ameamua kufanya kazi usiku na mchana, hatua ambayo imeongeza kasi ya ujenzi huo na anaamini kazi hiyo itakamilika kwa wakati.
Majaliwa amemtaka mshauri mwelekezi wa mradi huo ambaye ni M/SCONS AFRIKA LIMITED na FB Consultant wa Dar es Salaam asimamie kwa karibu ili kujiridhisha maelekezo yote yaliyopo kwenye michoro ya ujenzi huo yanazingatiwa na mkandarasi.
Amesema Serikali ya Tanzania imeamua kujenga machinjio hayo ya kisasa ya Vingunguti baada ya kugundua wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake katika machinjio hayo, walikuwa wakifanya kazi zao kwenye mazingira duni na nyama iliyokuwa ikitoka kwenye machinjio hayo ilikuwa haikubaliki kwenye soko la nje ya nchi.
“Uamuzi wa Serikali kujenga machinjio haya, utaifanya nyama inayotoka hapa ikubalike kwenye masoko ya nje ya nchi, hatua ambayo itaongeza mzunguko wa fedha kwenye eneo hili wakati Serikali na manispaa watanufaika kwani kutakuwa na ongezeko la makusanyo ya kodi,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu pia ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Manispaa ya Ilala wafanye mazungumzo na uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili ijengwe reli ya mchepuko kutoka reli ya kati kwenda kwenye machinjio ya Vingunguti ili mifugo iingizwe moja kwa moja kwenye machinjio hayo badala ya kuteremshiwa Pugu halafu ikapelekwa kwa magari.
Amewahakikishia wafanyabiashara wote wanaoendesha shughuli zao kwenye machinjio hayo kuwa ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti hautawafanya wapoteze fursa zao za biashara au kuajiriwa kwenye eneo hilo kwani machinjio hayo yatafungua fursa zaidi za biashara na ajira kwao.
Amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala wahakikishe wanaushirikisha uongozi wa wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake wa Vingunguti ili wanachama wao wenye sifa za kuajiriwa, waajiriwe na pia wawaandalie mazingira ya kufanya biashara mbalimbali karibu na machinjio hayo.
Akizungumzia soko na bei duni ya ngozi za mifugo nchini, Waziri Mkuu amekemea tabia ya wafugaji ya kuweka alama kwenye ngozi za mifugo yao hasa ng’ombe kwani kufanya hivyo kunashusha thamani ya ngozi za Tanzania badala yake amewataka waweke alama za hereni kwenye masikio ya mifugo yao ili kulinda ubora wa ngozi za mifugo yao.
Amesema Serikali tayari imekwishampata mwekezaji kutoka Misri ambaye amekubali kuwekeza kwenye kiwanda cha ngozi cha Mwanza hatua ambayo italihakikishia Taifa soko la ngozi.
Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri amesema ujenzi wa machinjio hayo ulianza Julai 8, 2019 na mkandarasi alitakiwa akamilishe ujenzi huo ifikapo Januari 6, 2021. Amesema kufuatia agizo la Rais Magufuli alilolitoa Septemba 16, 2019 ujenzi huo unatakiwa ukamilike ndani ya miezi mitatu yaani ifikapo Desemba 31, 2019.
Shauri amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo itagharimu Sh12.49 bilioni ambapo Sh8.52 bilioni ni ruzuku kutoka Serikali Kuu na Sh3.97 bilioni zimetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na kwamba ujenzi wa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 60.
Akisoma risala ya Ushirika wa Wafanyabiashara ya Mifugo na Mazao yake wa Vingunguti (UWAMIVI), mwenyekiti wao, Joel Meshaki ameiomba Serikali ya Tanzania iwaandalie wafanyabiashara hao eneo mbadala la kufanyia shughuli zao ili ajira yao isipotee.
Amependekeza kwa Waziri Mkuu maeneo matatu yaliyoko karibu eneo hilo, ambayo yangewafaa wafanyabiashara hao wakati watakapoondoka kwenye maeneo yao sasa yanapojengwa machinjio ya kisasa kuwa ni Dampo la zamani ambalo kwa sasa halitumiki, eneo la Wizara ya Kilimo ambalo kwa sasa ni sehemu ndogo tu inayotumika na jengo la Kilimo ambalo kwa sasa linatumika kama ghala.
Amesema idadi ya mifugo inayochinjwa katika machinjio hayo kwa sasa ni ng’ombe 550 hadi 600 kwa siku za kawaida na siku za sikukuu ni ng’ombe 1,000 hadi 1,500.
“Halmashauri yetu ya Ilala hukusanya zaidi ya sh. milioni 118 kwa mwezi wakati Serikali Kuu hukusanya milioni 117 kila mwezi,” amesema Meshaki.