Dodoma. Serikali imesema imekwishaanza mazungumzo na mataifa makubwa kwa ajili ya kununua korosho za wakulima ambazo minada ilishindikana.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa kauli hiyo bungeni leo Alhamisi Novemba 8, 2018 wakati akijibu swali la papo kwa hapo kutoka kwa mbunge wa Mtwara Mjini (CUF) Maftaha Nachuma.
Waziri Mkuu amekiri kuwepo kwa changamoto katika mauzo ya korosho katika masoko makubwa duniani ambako kumepelekea kupungua kwa bei.
Katika swali lake, Nachuma ametaka kujua ni kwa nini minada ya zao hilo ilikwenda kwa kusuasua hata wakulima kushindwa kuuza mazao yao.
Majaliwa amesema Serikali iliweka utaratibu mzuri kwa wanunuzi kununua kwa ushindani hali iliyofanya bei hiyo kupanda katika kipindi cha mwaka jana.
"Changamoto ni soko la kidunia, lakini hata leo hii Waziri wa Kilimo atakwenda kuzungumza na wanunuzi wengine muda mfupi ujao," amesema Majaliwa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewashukuru wakulima kwa kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu na akaomba wabunge kuendelea kuwatuliza wakulima.