Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa atoa maelekezo uzalishaji mafuta ya kula nchini

237928a7cc0db1c3de8d7a171c30442a.png Majaliwa atoa maelekezo uzalishaji mafuta ya kula nchini

Mon, 14 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Kilimo na Maafisa Ushirika nchini washirikiane katika kusimamia kilimo cha zao la alizeti kuhakikisha nchi inaondokana na utegemezi wa kuagiza mafuta ya kula kutoka nje.

Ametoa agizo hilo leo Jumapili wakati akizungumza na wadau wa zao la alizeti katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Mafunzo ya Kanisa Katoliki, Mkoani Singida. Amesema hakuna sababu ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje kwa sababu nchi ina ardhi nzuri pamoja na nguvu kazi ya kutosha.

Majaliwa amesema, "Lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji na tija kwa kuimarisha utafiti, huduma za ugani, upatikanaji wa mbegu bora na viuatilifu, kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo, kuwajengea uwezo wazalishaji kuhusu kanuni za kilimo bora, kuanzisha mfumo imara wa ugharamiaji wa mazao ya mafuta kwa kushirikisha taasisi za fedha."

"Ni matarajio ya Serikali kuwa mikakati hiyo itawezesha kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 649,437 hadi tani 1,500,000 za alizeti zitakazochangia upatikanaji wa mafuta kwa takribani tani 300,000 ifikapo 2025. Pia Serikali imeendelea kuwekeza katika taasisi zinazohusika na utafiti na uzalishaji wa mbegu ili kuongeza tija."

Waziri Mkuu amesema mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kuwa ni tani 650,000 na uzalishaji wa ndani ni wastani wa tani 290,000 sawa na asilimia 45 ya mahitaji kwa mwaka. Nchi hulazimika kuagiza wastani wa tani 360,000 hadi tani 400,000 kwa mwaka kufidia upungufu huo.

Amesema uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje kwa mwaka hugharimu takribani Sh bilioni 474. Amesema,"Fedha hizi ni nyingi kama tungelikuwa tunajitosheleza katika uzalishaji wa mafuta hapa nchini, zingeokolewa na kuelekezwa kwenye maeneo mengine ikiwemo uboreshaji na utoaji wa huduma za afya, elimu na miundombinu."

Aidha Waziri Mkuu amesema kutokana na umuhimu wa mafuta ya kula, Serikali imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta yakiwemo ya chikichiki, alizeti, pamba, karanga na ufuta ili kujitosheleza na kuondokana na uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imeweka mkakati wa kuboresha huduma za ugani kwa kuongeza bajeti ili kuhakikisha wakulima wa zao la alizeti wanalima kilimo bora na kuongeza tija kwenye uzalishaji.

Chanzo: www.habarileo.co.tz