Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa atoa hofu wakulima wa korosho

4b83cfe304508457a6b31ac8c9877073.jpeg Majaliwa atoa hofu wakulima wa korosho

Fri, 4 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wakulima wa korosho hawatakatwa Sh 110 kwa kila kilo ya korosho kwa ajili ya pembejeo.

Majaliwa alisema jana bungeni Dodoma kuwa, serikali imezungumza na benki ziwakopeshe wakulima wanunue pembejeo zinazohitajika katika mnyororo wa uzalishaji zao hilo.

"Hakuna kukatwa Sh 110 kwa ajili ya kupata pembejeo, waruhusiwe kuchukua pembejeo katika awamu zote nne katika maeneo kabla ya kufikia uzalishaji wa zao hilo," alisema Majaliwa.

Akaongeza; "Kiwango cha mbolea kilichoagizwa kinatosha wakulima katika maeneo yao na kitatosha awamu zote nne kufikia uzalishaji."

Majaliwa alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CCM), aliyetaka kujua serikali inasema nini kuhusu taharuki iliyoibuka kwenye mitandao kuhusu hatima ya zao la korosho.

Alisema hata yeye amesikia kupitia mitandao kuhusu taharuki hiyo iliyotokana na vikao vinavyofanywa na wizara ili kuweka uratatibu mzuri wa wakulima wa zao hilo kupata pembejeo.

“Ukweli ni kwamba Wizara ya Kilimo imekuwa ikifanya vikao mara kwa mara ili kufikia hatua nzuri ya kufikia kila mkulima…” alisema Majaliwa.

Alisema mkutano utafanyika Juni 6, mwaka huu ambapo wakulima, vyama vya ushirika, viongozi wa serikali na wabunge wataalikwa na kujadili namna bora ya kupata pembejeo hizo.

Aliwataka wananchi kuendelea kupokea pembejeo kwa ajili ya mnyororo wa uzalishaji zao hilo.

Kuhusu benki, Majaliwa alisema licha ya kusimama mwaka jana kwa kuhofu kwamba wasingeweza kulipwa na wananchi, mwaka huu zinatakiwa kuendelea kutoa mikopo kwa wakulima.

Alisema benki zinaendelea kutoa mikopo kwa ajili ya wananchi kupata pembejeo zikiwemo dawa za kupalilia, kupalilia, kulima na huduma nyingine katika zao hilo la korosho hivyo wakulima waende kukopa.

Alitaka wananchi wawe na imani na serikali kwamba inafanya utaratibu mzuri kuhakikisha wanazalisha zao hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz