Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema umefika wakati wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuanza safari za Mauritius ili kuvutia watalii zaidi.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Agosti 28, 2019 alipokutana na waziri mkuu wa nchi hiyo, Pravind Kumar nchini Japan wakati akiwakaribisha wafanyabiashara wa Mauritius kuwekeza Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu leo inaeleza kuwa wafanyabiashara hao wanaweza kuwekeza katika uzalishaji wa sukari, uvuvi na kujenga viwanda vya nyuzi za pamba na nguo.
Majaliwa amesema kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja kwenda Mauritius kutachangia kuwahamasisha watalii kuwekeza nchini.
“Umefika wakati wa ATCL kufikiria kuhusu safari za kwenda Mauritius ili kuwarahisishia wanaokwenda kufanya utalii wa fukwe katika nchi hiyo inayofanya vizuri katika sekta hiyo na kwa sababu Tanzania ina fukwe za bahari na maziwa kupitia ushirikiano huo utatuletea tija,” amesema.
Naye Pravind ameihakikishia Tanzania kuwa nchi hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na wizara na taasisi zinazohusika na uwekezaji nchini.
Habari zinazohusiana na hii
- Mamia waandamana Dar kushinikiza ndege ya Tanzania iliyozuiwa Afrika Kusini kuachiwa
- Polisi yawakamata wanaodaiwa kuratibu maandamano kudai ndege ya Tanzania kuachiwa