Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa apiga marufuku kahawa isiyokobolewa kusafirishwa nje ya nchi

34959 Majaliwa+pic Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa kahawa isiyokobolewa nje ya nchi ili kuiongezea thamani kabla ya kuingizwa sokoni.

 

Pia ameziagiza halmashauri zinazolima zao hilo nchini kuwa na kitalu chenye miche zaidi ya laki mbili ifikapo mwisho wa mwezi ujao.

 

Akizungumza na wadau wa kahawa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma jana Ijumaa Januari 4, 2019, Majaliwa alisema kuanzia sasa kahawa yote itakayozalishwa nchini ni lazima iongezewe thamani na hakuna kahawa yenye maganda itakayoruhusiwa kuuzwa nje ya nchi.

 

“Hairuhusiwi kutoa kahawa nchini na kuiuza nje ya nchi ikiwa bado na maganda, ni lazima iongezewe thamani ndipo ipelekwe katika masoko ya nje ya nchi ili iuzwe kwa bei nzuri, hii itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani na kulinda uwekezaji wa viwanda uliofanyika nchini,’’ alisema Majaliwa.

 

Kuhusu madeni ya wakulima, aliwaagiza watendaji wote wa Amcos waliohusika kutafutwa ili walipe.

 

“Kwa sasa Serikali haina taratibu za kununua madeni ya chama chochote cha ushirika. Kuendelea na utaratibu huo kunachochea viongozi wa ushirika kufuja mali za ushirika. Lazima watambue ukifuja fedha za wanaushirika, Serikali iko na wewe,” alisema

 

Alisema Serikali ya awamu ya tano haitarudi nyuma katika msimamo wake wa kuwasimamia wakulima ili nao waweze kunufaika na kazi kubwa wanayoifanya.

 

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa Amcos wahakikishe wakulima wote wanasajiliwa na taarifa zao ikiwemo ukubwa wa mashamba, kiasi cha uzalishaji na mahali walipo zinatunzwa vizuri katika kompyuta.

 

Pia, Waziri Mkuu alimuagiza Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma akague Amcos zote na kujiridhisha kama ziko hai na kwenye tatizo la uongozi aitishe uchaguzi.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema minada yote ya kahawa itafanyika kwenye maeneo yanayolima ambayo yamegawanywa katika kanda za Moshi, Kagera,  Songwe na Mbinga. 

 

Alisema lengo ya kufanya minada hiyo katika maeneo yanayolima kahawa ni kuongeza uwazi katika biashara hiyo na kuwawezesha wakulima kujua bei ya mnada na kulipwa kwa wakati.

 

Alisema mkulima anaruhusiwa  kupeleka kahawa katika mnada wowote nchini ilimradi azingatie sheria na taratibu husika 

 

Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha zao la kahawa ili kila mmoja anayehusika na zao hilo akiwemo mkulima aweze kunufaika na kuongeza tija.

 

Kwa upande wao, wadau walifurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kulisimamia zao kwa ukaribu na hasa baada ya kutangaza minada yote ya kahawa kufanyika katika maeneo yao na kwa uwazi.



Chanzo: mwananchi.co.tz