Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa ahamasisha kilimo cha parachichi kuchochea uchumi

Avocado Hass Parachichi Majaliwa ahamasisha kilimo cha parachichi kuchochea uchumi

Tue, 9 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wana-Iringa na Watanzania kwa ujumla waingie kwenye kilimo cha parachichi kwa kuwa zao hilo linachochea ukuaji wa uchumi.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, serikali ilikuwa ikitafuta masoko kwa ajili ya maparachichi yanayozalishwa nchini badala ya kutegemea nchi jirani pekee.

“Tumeshapata soko la moja kwa moja kwa ajili ya maparachichi yetu nchini China na India na tumegundua ya kwetu yana thamani kubwa na ubora wa hali ya juu ukilinganisha na maparachichi kutoka nchi nyingine.”

Alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali baada ya kukagua mradi wa kitalu cha miche bora ya parachichi unaomilikiwa na kikundi cha vijana cha Chilongola, kata ya Upendo, Mafinga Mjini, mkoani Iringa.

Aliwataka Watanzania waingie kwenye mpango wa kuzalisha miche ya zao hilo ili kuongeza idadi ya uzalishaji wa maparachichi. “Maparachichi yetu

yana ubora mkubwa. Na hii ni baada ya kupima udongo nchini kote na kubaini kuwa tuna maeneo yenye udongo unaofaa kwa kilimo hiki,” alisema.

Akizungumzia suala la barabara kama lilivyowasilishwa na wana kikundi hao, Waziri Mkuu alisema miundombinu ya barabara za kwenda mashambani linaratibiwa vizuri na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).

Kuhusu suala la kukosa mlango wa malimbichi bandarini, alisema analipokea na kuahidi kuwa atalifuatilia.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, alisema serikali imeshasaini mkataba na kampuni ya Afac Engineering ambayo itajenga kiwanda cha kusindika maparachichi katika eneo la Nyololo na katika awamu ya kwanza, Sh. bilioni 3.4 zitatumika.

“Wana-Mufindi ni watu wanaolima sana. Mbunge wenu amesimamia ahadi ya Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kujenga kiwanda cha kusindika maparachichi. Mkataba ulisainiwa na kabla ya Ijumaa ijayo, tutamkabidhi eneo mkandarasi ili aanze kazi,” alisema.

Kuhusu kusuasua kwa zao la chai, alisema serikali inatambua changamoto katika kiwanda cha DL, lakini imeshafanya uamuzi wa kukinunua kiwanda hicho na kukikabidhi kwa wakulima wadogo wa chai wa Mufindi ili wakiendeshe kupitia ushirika wao.

Kuhusu soko la mahindi, Silinde aliwataka wananchi hao wajiandae kuuza mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuanzia Julai 10, mwaka huu na kuahidi kuwa bei itakuwa nzuri. Hata hivyo, hakutaja bei hiyo.

Akifafanua zaidi, alisema: “Kutoka Zambia, tumepokea oda ya tani 650,000 za mahindi. Nchi jirani ya Congo (DRC) nao wametaka tani 500,000, lakini wanataka tuwape tani 200,000 za awali. Kwa hiyo, jiandaeni kuuza mahindi kuanzia tarehe 10 Julai, 2024.”

Mkurugeni wa kampuni ya Chilongola Agroforestry & Livestock, Andrew Salika, alisema kikundi chao kilianza mwaka 2020 kwa kuzalisha miche 9,000 na sasa wana miche 250,000 iliyo tayari kwenda sokoni. “Lengo letu ni kuongeza idadi ya miche bora ambapo mahitaji ni miche 730,000 kwa msimu mmoja,” alisema.

Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi alisema mji wa Mafinga ni miongoni mwa iliyo kwenye mradi mkubwa wa maji wa miji 28 nchini, lakini umefikia asilimia 18 pekee kutokana na kusuasua kwa kasi ya mkandarasi.

Aliiomba serikali isimamie kwa karibu ujenzi wa barabara ya Mafinga hadi Mgololo kwa kuwa Wilaya ya Mufindi inabeba uchumi wa mkoa mzima wa Iringa. “Barabara hii ikiisha, itarahisisha sana usafirishaji wa mazao ya wakulima na kuwa mkombozi wa wananchi wengi,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, alimweleza Waziri Mkuu kwamba wilaya hiyo ina ekari 800,000 ambazo ni miti pekee na kati ya hizo, 500,000 ni za miti ya kupandwa. Alisema wilaya hiyo ina viwanda 40 vya kuchakata mazao ya miti pamoja na mazao ya kilimo kama chai na pareto.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live