Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aahidi mikakati kuongeza ajira za utalii

1a02d8d1a61a7cbd533a22ff9716f3d6 Majaliwa aahidi mikakati kuongeza ajira za utalii

Mon, 7 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya utalii kwa kusimamia mikakati ya kukuza vivutio ili kuhakikisha Watanzania wakiwemo wakazi Arusha wananufaika kwa kupata ajira.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imeweza kupata mafanikio katika sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi 1,510,151 mwaka 2019.

Aliyasema hayo alipohutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Relini jijini Arusha ambako alimuombea kura mgombea urais kupitia chama hicho John Magufuli, mgombea ubunge jimbo la Arusha, Mrisho Gambo na wagombea udiwani.

"Sekta ya utalii ina umuhimu mkubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi hususani kwa vijana kwa sababu vijana wengi wameajiriwa na kujiajiri kupitia sekta ya madini. Serikali inawahakikisha kwamba itaendelea kuboresha mazingira ili kuweza kuvutia watalii wengi zaidi kuja nchini."alisema Majaliwa juzi jioni.

Alisema kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali katika sekta hiyo mapato yatokanayo na shughuli za utalii nchini yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 1,901.95 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 2,612.99 mwaka 2019.

Waziri Mkuu alisema mafanikio yote hayo yanatokana na uongozi thabiti na makini wa Rais Magufuli, hivyo amewaomba wana Arusha na Watanzania kwa ujumla kumchagua tena ili aweze kutekeleza mikakati mingine.

"Ndugu wanaArusha na Watanzania wote sina shaka kwamba mtakubaliana na ombi langu la kuwataka tumchague tena Rais Dk Magufuli kwa sababu mnapenda maendeleo na kwa Tanzania mtu atakayewaletea maendeleo si mwingine bali ni Dk John Magufuli tujitokeze kwa wingi kumpigia kura."alisema Majaliwa.

Akizungumzia kuhusu Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 alisema inaielekeza Serikali ya CCM kutekeleza mikakati ya kuboresha sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kukuza wigo wa bidhaa na mazao ya utalii.

Ilani imeelekeza Serikali ihakikishe inaongeza idadi ya watalii hadi 5,000,000 mwaka ifikapo 2025 na kuongeza mapato kutoka Dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani bilioni 6.0 mwaka 2025.

Chanzo: habarileo.co.tz