WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ikamilishe utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ili kuuwezesha kila mkoa kujua bidhaa hiyo inapaswa kuuzwa kwa bei gani, kwa nia ya kuondoa upandishwaji holela unaofanywa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.
Pia, ametoa onyo kwa mawakala wa saruji, kutoficha bidhaa hiyo kwa lengo la kupandisha bei kwa sababu kitendo hicho ni sawa na uhujumu uchumi, hivyo watakaobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana alipozungumza na wakuu wa mikoa, Katibu Mkuu Viwanda na Biashara, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, maofisa biashara wa mikoa, mawakala wa saruji walioko mikoani na wakurugenzi wa viwanda vya saruji.
Kikao hicho ambacho Waziri Mkuu alikiongoza kwa njia ya televisheni akiwa ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, kilihusu suala la bei na mwenendo wa upatikanaji wa saruji.
Majaliwa alisema lazima utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ukamilike ili kujua kila mkoa bidhaa hiyo inapatikana kwa kiasi gani.
“Mfano saruji inazalishwa Tanga au Dar es Salaam halafu Morogoro inauzwa kwa shilingi 28,000, sasa Kigoma itauzwaje, lazima kuwe na bei kikomo,” alisema.
Aliongeza kuwa suala hilo halihitaji kuundiwa bodi kwa sasa kwani vyombo vya kusimamia biashara vipo, wizara husika ipo, hivyo aliwataka wahusika wote wasimamie suala hilo kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.
Aliiagiza Tume ya Ushindani (FCC) ifanye ukaguzi ili kubaini kama bei za bidhaa hiyo ni shindani na zina tija kwa wananchi kwa sababu katika maeneo mengine hazina uhalisia na zinasababisha usumbufu nchini.
“Mawakala badilikeni na achaneni na tabia ya kuficha bidhaa kwa ajili ya kuzipandisha bei, ukikutwa unatengeneza mazingira ya kuifanya bidhaa isipatikane kwa lengo la kuipandisha bei huo ni uhujumu uchumi.
Ukikamatwa na bidhaa ambayo inatafutwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yako,” alisema.
Pia, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, watembelee viwanda mbali mbali ili kusikiliza matatizo yanayowakabili wenye viwanda na kushirikiana nao katika kuyapatia ufumbuzi.
Alisema licha ya bei ya saruji kuanza kupungua nchini, wakuu wa mikoa waendelee kufanya ukaguzi na kufuatilia mwenendo wa bei ya saruji ili kubaini kama bei wanayouziwa wananchi ni halali na wahakikishe bei ya bidhaa hiyo inaendelea kushuka.