Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Wawekezaji zitumieni fursa

152304f9d0e138c62a1c2da573a9a20a Majaliwa: Wawekezaji zitumieni fursa

Mon, 17 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa rai kwa wawekezaji wachangamkie fursa kwa kuangalia maeneo mazuri ya kuwekeza au kupanua uwekezaji wao.

Ametoa rai hiyo jana alipozungumza na wakazi wa Namichiga, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, waliohudhuria uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda cha samani cha Saw Mill and Furniture Processing Industry.

Baada ya kuzungumza hapo Majaliwa alikagua eneo la ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho wilayani humo.

"Kwa upande wa viwanda, tusiishie tu kwenye korosho, tuone pia namna ya kuwa na viwanda vya kuchakata ufuta, mbaazi na mazao mengine yanalimwa kwa wingi kwenye maeneo yetu ili kijihakikishia soko na upatikanaji wa ajira."alisema.

Waziri Mkuu alisema, kiwanda hicho ni cha kwanza Ruangwa hivyo wakazi wa Namkonjera na vijiji vya jirani wapime ardhi yao ili watu wanunue viwanja na kuanza kujenga.

"Kujengwa kwa kiwanda cha kutengeneza samani na baadaye kiwanda cha kubangua korosho, kutahamasisha uzalishaji wa mazao ya kilimo na misitu pamoja na kuimarisha mnyororo wake wa thamani. Endapo mtajipanga vizuri kwa kujenga viwanda vya kuongeza thamani kwenye zao la korosho, wilaya hii itakuwa kinara kwenye uzalishaji wa zao hilo,"alisema Majaliwa.

Alisema uwekezaji huo utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuanzisha na kuendeleza viwanda ili kukuza uchumi, kuleta maendeleo endelevu, kuongeza ajira, na kupunguza umasikini kwa Watanzania.

Majaliwa alisema, kuimarika kwa uzalishaji hususan kupitia ujenzi wa viwanda, kumekuwa chachu ya upatikanaji wa huduma hasa kutokana na kuimarika mapato ya Serikali na ajira kwa Watanzania.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imefanikiwa kuimarisha sekta za kiuchumi na uzalishaji ikiwemo viwanda na biashara.

"Katika kipindi hicho jumla ya viwanda vipya 8,477 vimejengwa na kuchangia kuzalisha ajira mpya 482,601," alisema Majaliwa.

Alisema sekta ya viwanda imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kwamba, kwa mwaka 2019 ilikua kwa asilimia 8.5 ikilinganishwa na asilimia 8.05 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 0.45.

"Mchango huo unakwenda sambamba na kuimarika kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani. Kwa mfano, mwaka 2019 bidhaa za viwanda zilikuwa na thamani ya shilingi trilioni 10.2 ikilinganishwa na shilingi trilioni 9.6 mwaka 2018 sawa na ukuaji wa asilimia 5.8," amesema.

Alisema maendeleo ya uwekezaji katika sekta ya viwanda yameongeza uzalishaji wa bidhaa zikiwemo za chuma, saruji, vigae, nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi, kusindika nyama, chakula, mbogamboga na matunda, maziwa, mafuta ya kula, sukari, vifungashio, mbolea, dawa za binadamu, sabuni na sigara na ubanguaji wa korosho.

Katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Kilimo, Omar Mgumba alisema uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda hicho ni matokeo ya msisitizo wa Rais John Magufuli na usimamizi wa karibu wa Waziri Mkuu kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Magira Masegesa alisema kiwanda hicho kinamilikiwa na kampuni ya wazawa ya Orascom Construction and Engineering Company(T)Ltd ikishirikiana na kampuni tanzu yaYukos Entreprises yenye makao makuu jijini Dar es Salaam, na kimeajiri wafanyakazi 150.

Alisema shilingi bilioni 5 zimewekezwa katika kiwanda hicho kwenye awamu ya kwanza.

Chanzo: habarileo.co.tz