Lindi. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Sh222bilioni zimelipwa na Serikali kwa wakulima wa zao la korosho.
Amesema wakulima walioanza kulipwa ni wale wenye kilo zisizozidi 1,500 na kwamba wenye kilo zaidi ya 1,500 Serikali inaendelea na uhakiki wawe na subira watalipwa.
”Fedha zipo hakuna mkulima ambaye atapoteza haki yake wote watalipwa. Tunaendelea na uhakiki kwa wale wenye korosho nyingi ili kubaini kama hawajanunua kangomba,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 30, 2018 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nandagala ‘A’ baada ya kufungua ofisi ya CCM katika kata ya Nandagala.
Amesema baadhi ya watu wamekutwa na kilo zaidi ya 1,500 na kushindwa kuonyesha mashamba yao ya mikorosho hali inayodhihirisha kwamba wamenunua kupitia kangomba.
Waziri Mkuu amesema baadhi ya waliokutwa na korosho nyingi ni vijana wadogo ambao hawana hata uwezo wa kifedha hivyo Serikali itahakikisha inawakamata watu wanaowatuma.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo, kwamba biashara ya kangomba lazima idhibitiwe.
Majaliwa ambaye leo ameanza ziara ya kikazi wilayani Ruangwa mkoani Lindi amesema zoezi la ulipaji kwa wakulima wa korosho linaendelea, wakulima wawe na subira.
Serikali iliamua kununua korosho zote za mwaka huu baada ya kubaini wafanyabiashara wamepanga kuwadhulumu wakulima kwa kupanga kununua kwa bei ndogo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametembelea eneo la ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Matambalale wilayani Ruangwa na kuwataka wahakikishe ujenzi unakamilika
Amewataka wananchi wa kata hiyo kushirikiana na kuhakikisha wanachangia nguvu kazi katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili mwakani wanafunzi waanze kusoma.
Amesema wanafunzi zaidi ya 200 wamefaulu na hawana pa kwenda ni lazima ujenzi wa shule zote za sekondari za Matambalale, Chibura na Ruchelegwa ukamilike.
Waziri Mkuu amesema hadi Januari 10, 2019 shule hizo lazima ujenzi wake ukamilike ili wanafunzi waanze kusoma.