Mkurugenzi Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amesema suala la ulipaji kodi limekuwa na ukakasi kwa wananchi sio wa Tanzania tu bali maeneo mengi duniani licha ya kwamba ni jambo la lazima kwa ajili ya manufaa ya Taifa na maendeleo ya nchi.
Kayombo amesema hayo leo Jumatano, Desemba 15, 2021 wakati akizungumza mambo mbalimbali yahusuyo ulipaji kodi kupitia Kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia +255 Global Radio.
"Masuala ya magari ni sehemu mojawapo tunayohusika nayo ikiwemo usajili wa umiliki wa vyombo vya magari. Kuna taratibu za msingi ambazo lazima mtu azifuate ili kukamilisha kuhamisha umiliki wa chombo cha moto.
"Suala la kodi limekuwa likileta ukakasi si Tanzania tu, bali maeneo mengi duniani, hata Yesu aliulizwa, 'Je, ni halali kulipa kodi?' lilikuwa swali la mtego kujaribu kutafuta njia. Akawaambia ya Mungu mpe Mungu na ya Kaisali mpe Kaisali.
"Ili Serikali iweze kutimiza majukumu yake ya kimaendeleo unatakiwa ulipe kodi, hata kiimani kuna Zaka. Hivi vinakuwa vinatokana na kipato ambacho mtu anakipata kutokana na shughuli halali za kiuchumi.
"Huwezi kusema utajenga barabara yako peke yako, huwezi kujenga Hospitali yako peke yako, lazima tuchangie kwenye mfuko wa Serikali kisha Serikali itufanyie maendeleo.
"Kodi ni mchango wa lazima ambao unatokana na mapato halali ambayo mtu anayapata, lakini lazima tujenge uelewa kwa wananchi ili kuwajengea uhiari wa kulipa kodi," -Richard Kayombo, Mkurugenzi Huduma na Elimu kwa Mlipakodi (TRA).