Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jafo aanika wafanyabiashara wa nyama 'wanavyowapiga' wateja

Jafooo 77 Waziri Dk. Selemani Jafo alipotembelea kituo cha kupimia ujazo wa malori Misugusugu

Sat, 13 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo amefichua namna wauza nyama buchani wanavyocheza na mizani na kuwaibia wateja wao kwa kuwawekea vipimo visivyo sahihi.

Alibainisha mbinu hizo jana alipotembelea kituo cha kupimia ujazo wa malori cha Wakala wa Vipimo (WMA) cha Misugusugu, mkoani Pwani, akiwa ameambatana na Naibu Waziri wake, Exaud Kigahe na Naibu Katibu Mkuu wizarani, Balozi Dk. John Simbachawene.

"Ile mizani ya zamani yenye sufuria upande mmoja na jiwe kwingine kila ukiondoka unakuta kaweka jiwe la ujazo wowote, hawezi kuuacha mzani ukiwa bila jiwe. 

"Ukiingia buchani anakuuliza unataka kilo ngapi, ukisema tu anatoa jiwe alilokuwa ameweka anaweka la ujazo unaotaka wewe, ule ni ujanjaujanja tu wa kukuibia.

"Anaweka jiwe muda wote kwa sababu anajua lisipokuwapo mizani haiwezi kuwa sawa, kwahiyo mteja anaweza kushtukia kwa sababu akitoa jiwe tu mzani unaangukia kwenye lile sufuria kubwa upande mwingine. Kwahiyo, unapimiwa kilo moja wakati mwingine robo nzima imeibiwa.

"Sijui kama wenzangu mnayaona haya lakini inawezekana wengine ni wa mboga nane hamjawahi kuishi maisha ya uswahilini, hivyo hamwezi kuelewa hiki ninachosema, lakini ndiyo hali yenyewe," alisema Waziri Jafo.

Alisema wapo baadhi ya wafanyabaishara ambao wamekuwa wanatumia mbinu zingine za kuwaibia wateja ikiwamo ya kukandamiza mizani kwa kutumia kisu, wengine wakitumia sumaku.

Alisema WMA ina kazi kubwa ya kupambana na wizi huo, akiwataka viongozi wake kushirikisha maofisa biashara wa mikoa na wilaya kuwatafuta na kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaohusika na vitendo hivyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Jafo alielekeza watendaji walio chini yake kumaliza hujuma zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaopunguza ujazo wa mifuko  ya saruji.

Alisema kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu kupungua kwa ujazo wa mifuko hiyo ya saruji ambayo inapotoka kiwandani inakuwa na ujazo sahihi wa kilo 50, lakini inafika kwa wateja ikiwa na wastani wa kilo 40 au 45.

"Inawezekana ikawa ni kazi kubwa, lakini sisi ndiyo tumepewa wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na vipimo sahihi, mtendaji mkuu na timu yako mnapaswa kusimamia kuhakikisha hujuma hizi zinakomeshwa," aliagiza Waziri Jafo.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Exaud Kigahe alimpongeza Dk. Jafo kwa kuanza kazi kwa kasi baada ya kuapishwa hivi karibuni na kumwahidi kuwa atampa ushirikiano katika utendaji kazi wake.

Alisema taasisi nyingi zilizo chini ya wizara hiyo zinafanya kazi ya kuweka mazingira mazuri ya wenye viwanda na biashara kustawi na kulinda ushindani kwenye biashara na walaji wa mwisho ili wanaouza wasiibiwe na wale wanaonunua wasiibiwe.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla alisema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na waziri na kuahidi kuyafanyia kazi katika muda uliopangwa.

Kihulla alieleza kuwa WMA kupitia kituo hicho  cha Misugusugu, ina uwezo wa kuhakiki mita za umeme, dira za maji na magari yanayotumika kusafirisha vimiminika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live